2017-01-19 16:06:00

L'Osservatore Romano: kioo cha maisha na utume wa Papa!


Gazeti la L’Osservatore Romano linalomilikiwa na Vatican, hivi karibuni limezindua tena Jarida linalotolewa mara moja kwa juma katika lugha ya Kiitalia, ili kuwawezesha wasomaji wake kuona kwa karibu zaidi maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni; mchakato wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; umuhimu wa kujikita katika kutafuta na kudumisha haki, amani na maridhiano duniani; majadiliano ya kidini na kiekumene kama nyenzo ya kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kati ya watu; nafasi na dhamana ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa.

Kimsingi haya ndiyo yaliyojiri wakati wa uzinduzi wa Jarida jipya la L’Osservatore Romano ambalo kwa sasa linachapishwa mara moja kwa Juma katika lugha ya Kiitalia. Uzinduzi huu umehudhuriwa na viongozi wakuu kutoka katika Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican chini ya uongozi wa Monsinyo Dario Eduardo Viganò. Shughuli nzima ikaratibiwa hapo tarehe 10 Januari 2017 na Dr. Grek Burke, Msemaji mkuu wa Vatican pamoja na Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu Msaidizi wa Vatican pamoja na Jopo zima la wahariri wakuu wa Gazeti la L’Osservatore Romano ambalo limekuwa mtam boni kwa zaidi ya miaka sabini sasa.

Askofu mkuu Becciu katika hotuba yake amesema, Gazeti la L’Osservatore Romano linatoa muhtasari wa maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Vatican katika ujumla wake. Jarida lilozinduliwa ni mwendelezo wa jitihada za Mama Kanisa kukutana na watu katika mazingira mbali mbali, ili kuwawezesha kusikia sauti ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika undani wake. Hii ni changamoto kubwa ya kiutendaji na kiuhariri kwani mwelekeo wa wengi kwa sasa ni kuchapisha magazeti katika mitandao ya kijamii, lakini kusoma gazeti katika hali ya utulivu, kuna utamu na raha yake anasema Askofu mkuu Becciu.

Mama Kanisa anapenda kuendelea kuwahimiza walimwengu kushikamana katika kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Ni mchakato unaowahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kuendeleza zawadi ya amani, haki, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Lengo mahususi ni kudumisha utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ulimwenguni. Kanisa linataka kuwa ni chachu ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama inavyojitokeza kwa sas anchini DRC. Juhudi za Baraza la Maaskofu Katoliki DRC zimesaidia kwa sasa kudhibiti mpasuko wa kisiasa na kijamii nchini DRC.

Gazeti la L’Osservatore Romano limekuwa na jicho la pekee katika maisha na utume wa wanawake ndani ya Kanisa kwa kuchapisha Jarida la Wanawake ndani ya Kanisa linalotolewa kila mwezi. Monsinyo Dario Edoardo Vigano, Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican anasema, yote haya ni sehemu ya mchakato wa mageuzi yanayoendelea kufanywa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican; kwa kubana matumizi lakini kwa kutoa nafasi kwa mang’amuzi mapya katika maisha na utume wa Kanisa. Changamoto kubwa kwa sasa kwa Gazeti la L’Osservatore Romano ni kuhakikisha kwamba, linatafuta njia mpya na bora zaidi za kuweza kulisambaza kwa wasomaji wengi zaidi. Gazeti hili litaendelea pia kuchapisha hotuba na nyaraka mbali mbali za Khalifa wa Mtakatifu Petro katika mtandao wake. Jarida hili litakuwa na sehemu kuu nne: Habari za Vatican; Matukio ya Kimataifa: Kitamaduni na Kidini. Lengo ni kuliwezesha Gazeti hili kuwa ni mahali pa watu kukutana kama anavyotaka Baba Mtakatifu Francisko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.