2017-01-19 14:54:00

Jubilei inawezesha huruma ya Mungu kukutana na udhaifu wa binadamu


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 19 Januari 2017 amekutana na kuzungumza na waandaaji wa Onesho la Mambo ya Kale kuhusu historia ya Maadhimisho ya Jubilei, waliokuwa wamesindikizwa na Bwana Pietro Grasso, Rais wa Seneti ya Italia. Amewashukuru na kuwapongeza kwa kuandaa Onesho hili lililokuwa kwenye Ofisi za Senate ya Italia kwa muda wa mwaka mzima, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Onesho hili ni Nyaraka muhimu sana katika Miaka Mitakatifu kuanzia tangu mwaka ule wa kwanza kabisa ulioitishwa na Papa Bonifasi VIII kwa Waraka wake wa Kitume “Antiquorum habet” yaani “Tunayo Mambo ya Kale”. Tangu mwaka 1300 na kuendelea, maadhimisho ya Jubilei yameendelea kuitajirisha historia ya mji wa Roma: kwa kuuwezesha mji wa Roma kuwa ni mjenzi mkuu wa ukarimu kwa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia; sanaa inayoonesha mambo msingi na huduma ya upendo. Lakini, jambo la msingi katika kila maadhimisho ya Jubilei ni waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukutana na wema na huruma ya Mungu katika maisha yao.

Wema na huruma ya Mungu inakutana na udhaifu wa binadamu, unaohitaji daima kugangwa na kuonjeshwa upendo na msamaha wa Baba wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu anatumia huruma ili kuonesha uweza na ukuu wake kwa binadamu! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwatakia mema wale wote waliojitaabisha kuandaa Onesho hili na ni matumaini yake kwamba, kila mmoja wao, ataendelea kuvutwa na mang’amuzi ya maadhimisho ya Jubilei, ili kudumisha matunda ya maisha ya kiroho endelevu na dumifu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie katika kukuza nia hii njema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.