2017-01-18 15:40:00

Wadominican wanatumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu


Shirika la Wadominican katika mkutano wake mkuu ulioadhimishwa kunako mwaka 2013 huko Trogir kwa ajili ya kupembua utume wa Shirika, wajumbe wa mkutano huo mkuu waliamua kufanyike maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wadominican duniani; maadhimisho ambayo yalianza kutimua vumbi kunako mwaka 2016. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 21 Januari, 2017, kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa jioni kwenye Kanisa kuu la Yohane wa Laterano, Jimbo kuu la Roma.

Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Kongamano la Kimataifa la Wadominican lililozinduliwa rasmi, Jumanne, tarehe 17 Januari 2017 kwenye Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, maarufu kama Angelicum, kilichoko mjini Roma. Lengo la kongamano hili ni kufanya upembuzi yakinifu na uelewa wa maisha na utume wa Wadominican katika ulimwengu mamboleo. Kukutana na kuendeleza mchakato wa ushirikiano miongoni mwa Wadominican kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuunda na kudumisha mtandao wa utume wa Shirika katika maeneo mbali mbali ya dunia pamoja na kufanya utambuzi wa maeneo mapya ambamo wanaitwa na kutumwa na Mama Kanisa ili kushiriki kikamilifu!

Wadominican katika kongamano hili la kimataifa wanataka kupyaisha mfumo na mtindo wa maisha na utume wao wa kuhubiri na kushuhudia Neno la Mungu kati ya Watu wa Mataifa. Wajumbe wanaendelea kuchambua ni sehemu zipi ambazo wamekuwa na nguvu zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na mapangufu yao katika utekelezaji wa dhamana hii kutoka kwa Mama Kanisa. Uwajibikaji na utayari wao kwa Kanisa; umuhimu wa Injili ya familia na changamoto zake ni mambo yanayoendelea kuchambuliwa kwa kina na mapana.

Kongamano hili pamoja na mambo mengine, linaendelea kujadili changamoto za wakimbizi na wahamiaji duniani; watu mahalia; majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani duniani. Dhamana na utume wa kuhubiri Injili mijini; Ibada ya Rozari Takatifu ambayo kimsingi ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi. Mada nyingine zinazojadiliwa ni pamoja na: utume Parokiani, elimu na uinjilishaji; mchakato wa Saramanca; Shule ya kuhubiri; masomo kama sehemu ya utume; haki msingi za binadamu; huduma kwa wanafunzi vyuo vikuu na wafungwa magerezani; huduma katika sekta ya afya na vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Mtindo wa maadhimisho ya Kongamano la Wadominican: Siku ya kwanza wanajadili kuhusu: utu wa binadamu kwa kuangalia haki, amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; wakimbizi na wahamiaji, watu mahalia pamoja na haki msingi. Siku ya pili, wanaangalia kuhusu mkutano kwa kupembua kwa kina na mapana mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; utamaduni wa kusikiliza kwa makini, elimu, vyombo vya mawasiliano ya jamii na ulimwengu wa mitandao ya kijamii. Siku ya tatu, wajumbe wataangalia utume wao katika Neno la Mungu, huduma ya kuhubiri mijini, utume Parokiani, huduma kwa wagonjwa na wafungwa. Mwishoni, watarejea kwenye tema ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 tangu Shirika la Wadominican lilipoanzishwa kwa kujikumbusha kwamba, wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hadi miisho ya duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.