2017-01-18 15:21:00

Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri: Shukrani, Toba na Matumaini


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, tarehe 31 Oktoba 2016 lilizindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, tukio ambalo lilimshirikisha Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wengine wakuu wa Makanisa. Tukio hili ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki la Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani katika kipindi cha miaka 50 iliyopita na matunda yake yanaanza kuonekana. Kilele cha Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri ni Mwaka 2017.

Kardinali Koch anakiri kwamba, licha ya umuhimu wa maadhimisho haya kama sehemu ya mchakato wa Uekumene wa maisha ya kiroho, ushuhuda, damu na huduma, lakini baadhi ya waamini waliyaona kuwa ni usaliti wa Mageuzi ya Kiluteri Duniani, mchakato endelevu! Mageuzi haya yalipofanyika kunako mwaka 1617, Ulaya ilijikuta ikimeguka kutokana na kinzani za kivita, mipasuko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kunako mwaka 1917, Martin Luther alisherehekewa na kukumbukwa kama Muasisis wa Lugha ya Kijerumani na shujaa wa vita. Kwa bahati mbaya, Ulaya ikajikuta inatumbukia katika Vita ya Kwanza ya Dunia iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Mahusiano kati ya Wakatoliki na Waluteri anasema Kardinali Kurt Koch yakawa na sura mbaya sana. Lakini, mchakato wa majadiliano ya kiekumene uliendelea kushika kasi na kwa namna ya pekee, baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hapa, mchakato wa majadiliano haya ukaanza kuchukua sura mpya, kwa kushiriki katika furaha, mateso na matumaini ya Wakristo wengine duniani! Kumbe, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni hatua muhimu katika majadiliano ya kiekumene kati ya Wakatoliki na Waluteri Duniani. Waamini wa pande zote mbili wanaweza kujifunza ili kurejesha na kuimarisha imani ya waamini kwa Kanisa la Kristo lengo kuu lililokuwa moyoni mwa Martin Luther wakati akianzisha cheche za mageuzi ya Kiluteri! Maadhimisho ya Mwaka 2017 yanalenga kukuza na kudumisha umoja wa kiekumene unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa la Kristo mintarafu mwanga wa Injili. 

Kuanzishwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani anasema Kardinali Kurt Koch ni njama za kisiasa zilizoteka mchakato wa mageuzi ya Kiluteri kunako karne ya XVI, kumbe, hii ni sehemu ya mapungufu ya mageuzi haya, kwani yalisababisha Umoja wa Kanisa la Kristo kumeguka. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakaona ile nia njema ya Mageuzi ya Kiluteri, wakalitaka Kanisa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kujenga tena Umoja wa Kanisa. Mwaka 2017 ni changamoto na mwaliko wa kurejea tena na tena katika wazo asilia la kutaka kulipyaisha Kanisa la Kristo, changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na Wakatoliki na Waprotestanti ili kusuka tena ule uhusiano na umoja wa Kiekumene unaofumbatwa katika imani na maisha ya Kiimani.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwahi kusema kwamba, Jubilei ya miaka 500 ya Magezui ya Kiluteri Duniani iwe ni fursa ya kwa waamini kukiri imani yao katika Fumbo la Utatu Mtakatifu pamoja na kuonesha utii kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, changamoto na mwaliko wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uekumene unaofumbatwa katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mwaliko wa kutoka katika vita na kinzani za kidini na kuanza kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Kanisa.

Jambo la kwanza katika maadhimisho ya Mwaka 2017 ni “kushukuru” kwa mchakato wa majadiliano ya kiekumene ulionzishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani likawa la kwanza kujiunga na mchakato huu na matunda yake ni mweleko wa upatanisho baada ya Makanisa haya mawili kuchapisha hati ya pamoja juu ya “Kuhesabiwa Haki ndani ya Kanisa” iliyotiwa mkwaju kunako mwaka 1999. Hii ni hati inayofumbata mambo msingi ya imani ya Kanisa, kumbe, hili ni jiwe la msingi la majadiliano ya kiekumene!

Ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwani hata Kanisa Katoliki limeweza kuyaangalia Mageuzi ya Kiluteri Duniani kwa jicho lenye mwelekeo chanya zaidi, licha ya changamoto ambazo bado zinapaswa kufanyiwa kazi zaidi. Martin Luther alikuwa amejikita zaidi katika taalimungu ya kuhesabiwa haki kwa njia ya neema na imani peke yake. Kumbe, neno la pili ni “kutambua” dhambi na mapungufu yaliyojitokeza kati ya Makanisa haya mawili, hivyo kuwa tayari kukiri na kuyajutia makosa haya, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi.

Mageuzi ya Kiluteri Duniani yametoa kipaumbele cha kwanza kwa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni Neno wa Mungu aliye hai! Neno la Mungu liwe ni chachu ya Umoja wa Wakristo duniani. Wabatizwa wote katika ujumla wao ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa! Hakuna tena sababu ya kutwangana ngumi na kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na misigano ya kiimani kama ilivyojitokeza kati ya Karne ya XVI hadi Karne ya XVII, Bara la Ulaya likachorwa kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Hapa kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mungu.

Papa Adriano VI kunako mwaka 1522 alikiri na kuungama makosa ya viongozi wa Kanisa Katoliki, dhamana iliyoendelezwa pia na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na viongozi wengine waliofuatia! Hiki kinapaswa kuwa ni kiini cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Waamini wajitahidi kutakasa kumbu kumbu zao za kihistoria, anasema Baba Mtakatifu Francisko ili makosa ya kihistoria yasiwe ni mzigo na kikwazo cha kujenga umoja na mshikamano wa Kanisa, kwani huruma ya Mungu inapaswa kuwa ni chachu ya umoja na mshikamano wa Wakristo duniani. Kumbe, huruma na msamaha iwe ni dira na mwongozo katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene duniani! Neno la tatu anasema Kardinali Kurt Koch ni ”matumaini” yanayobubujika kutoka katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Kanisa katika furaha na shukrani kwamba, licha ya mapungufu ya binadamu, Kanisa linaweza kusonga mbele ili kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika ukweli na uwazi.

Baada ya miaka 500 ya utengano, sasa ni wakati wa kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo, ili kunako mwaka 2030, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Baraza la Augsburg sanjari na Ilani ya Augustana, Wakristo wote waweze kukiri imani yao kwa Kristo Yesu. Kumbe, kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri ni mwanzo mpya katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: shukrani, toba na matumaini; mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko na viongozi wakuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani waliyashuhudia wakati wa kuzindua Sherehe hizi hapo tarehe 31 Oktoba 2016 huko Lund, nchini Sweden.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.