2017-01-18 15:06:00

Matumaini ya Umoja wa Wakristo yanajikita katika sala!


Mwishoni, baada ya kutafakari uhusiano wa dhati uliopo kati ya matumaini na sala, wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 18 Januari 2017 kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbusha waamini na mahujaji kwamba, tarehe 18 Januari 2017, Kanisa linaanza Juma la Sala kwa ajili ya Kuombea Umoja wa Wakristo ambalo linaongozwa na kauli mbiu ”Upatanisho: Upendo wa Kristo unatuwajibisha”.

Matumaini ya Umoja wa Wakristo yanafumbatwa hata katika sala. Haya ni matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya kama inavyoshuhudiwa kwa matukio mbali mbali katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika kipindi cha takribani miaka 50 iliyopita. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo wote kuanzia sasa hadi tarehe 25 Januari 2017 kuzidisha ari na moyo wa sala kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo! Injili inapaswa kuwa ni kiini kinachowaunganisha Wakristo kutoka katika lugha, jamaa na taifa; lakini wote hawa wanaishi imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, bado ana kumbuka sala ya kiekumene iliyofanyika mjini Lund, Sweden, tarehe 31 Oktoba 2016, kama sehemu ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Wakristo kwa sasa wanapaswa kuangalia mambo msingi yanayowaunganisha zaidi kuliko yale yanayowagawa na kuwatenganisha. Waamini waendeleze safari ya majadiliano ya kiekumene ili kupembua kwa kina na mapana mambo msingi yanayowaunganisha, ili hatimaye, kuyatolea ushuhuda unao onekana.

Barani Ulaya, imani kwa Kristo na Kanisa lake linaonesha matumaini kwani waamini wanategemeana na kukamilishana. Baba Mtakatifu anasema umoja na upatanisho ni mambo yanayowezekana. Hii ni dhamana ambayo Wakristo wanapaswa kuifanyia kazi kwa kuishuhudia katika uhalisia wa maisha yao. Baba Mtakatifu ameombea utashi wa umoja wa Wakristo na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aliwalinde waamini wote wanaotembea katika hija ya majadiliano ya kiekumene! Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya umoja na amani ili hatimaye, kujenga ulimwengu unaojikita katika udugu, haki na amani; upendo na mshikamano wa dhati unaotoa fursa kwa watu kusaidiana kwa hali na mali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.