2017-01-18 14:51:00

Matumaini ya Kikristo hujionesha katika hatari kwa njia ya sala!


Nabii Yona ni kielelezo cha matumaini na sala! Yona alijaribu kutoroka Neno na uso wa Mungu lakini akaambulia kumezwa tumboni mwa samaki na kukaa humo kwa muda wa siku tatu mchana na usiku, lakini alipokuwa tumboni mwa samaki yule akamlilia Mungu katika shida yake naye akamwitikia. Huu ni mwendelezo wa Katekesi juu ya matumaini ya Kikristo iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 18 Januari 2017. Nabii Yona alitaka kukimbia wajibu wa kutangaza na kushuhudia  mpango wa wokovu, lakini akajikuta anatumbukia tumboni mwa samaki, lakini anaokolewa na kuponywa na huruma ya Mungu katika maisha yake.

Kitabu cha Nabii Yona kimegawayika katika sura kuu Nne, lakini kimesheheni mafundisho makuu ya imani na matumaini anasema Baba Mtakatifu kwani Yona ni Nabii ambaye Mwenyezi Mungu anamtuma kwenda pembezoni mwa jamii katika mji wa Ninawi, ili kuwahubiria watu toba na wongofu wa ndani. Nabii Yona kama ulivyokuwa Mji wa Ninawi, alikuwa ni tishio kwa Yerusalemu, kumbe, alipaswa kufutiliwa mbali bila huruma badala ya kuokolewa. Nabii Yona alipotumwa na Mwenyezi Mungu kwenda kuwahubiriwa wananchi wa Ninawi alitambua utashi wa Mungu na akataka kukwepa dhamana na jukumu hili kwa kukimbilia mbali na uso wa Mungu. Akiwa njiani akabahatika kukutana na manahodha wapagani baada ya kumhoji sana wakamkata na kumtupa baharini. Kitendo hiki na kile cha wananchi wa Ninawi kutubu na kumwongokea Mungu, Baba Mtakatifu anasema, ndicho kiini cha tafakari juu ya matumaini ya Kikristo mbele ya hatari na kifo kwa kuonesha sala.

Katika patashika nguo kuchanika kutokana na machafuko ya bahari, kila mtu alikimbia kumlilia Mungu wake, lakini kwa bahati mbaya, Yona alikuwa ameuchapa usingizi ndani ya Merikebu! Akaamshwa kwa kishindo, ili aweze kusali na kumwomba Mungu wake ambaye angeweza kuwakumbuka na kuwaokoa. Mbele ya kifo anasema Baba Mtakatifu, mwanadamu anatambua udhaifu wake na umuhimu wa kuokolewa! Hofu ya kifo inaamsha ndani ya mwanadamu umuhimu wa kumtumainia Mwenyezi Mungu asili ya maisha, ili aweze kuwakumbuka na kuwaokoa! Haya ni maneno ya matumaini yanayogeuka na kuwa ni sala inayozima mahangaiko ya ndani na kusikika midomoni mwake anapoona kifo kinamkodolea macho!

Baba Mtakatifu anasikita kusema kwamba, wakati wa shida na magumu watu wengi wanashindwa kumkimbilia Mungu kwa kudhani kwamba, sala yao si kamili na wala haina umuhimu wowote mbele ya kifo. Lakini, Mwenyezi Mungu anatambua udhaifu wa binadamu ambaye mara nyingi anamkimbilia wakati wa kuomba msaada, lakini katika hali na tabasamu la kibaba, Mwenyezi Mungu anamjibu mwanadamu katika huruma.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Nabii Yona alipogundua dhamana na wajibu wake mbele ya Mwenyezi Mungu akajirusha baharini ili kuokoa maisha ya abiria wengine na kweli bahari iliyokuwa imechafuka ikatulia tuli kama “maji mtungini”. Woga wa kifo, ukawasukuma wapagani kumpigia Mungu magoti kwa sala pamoja na kuhakikisha kwamba, Nabii Yona anatekeleza dhamana na wajibu wake, kwa kukubali kujisadaka kwa ajili yao na hatimaye, akawasaidia kumtambua Mungu wa kweli kwa kumwabudu na kumshukuru. Manahodha wa merikebu walio walilia miungu yao kwa hofu ya kifo, wanamtambua na kumwona Mungu wa kweli, kiasi cha kumtolea sadaka na kumwekea ahadi zao. Matumaini yaliyowafanya wapagani kumlilia Mungu ili wasipotee yanajionesha kuwa na nguvu zaidi ya kile ambacho walikitumainia, yaani ufunuo wa Mungu aliyeumbwa mbingu na nchi!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, hata wananchi wa mji wa Ninawi waliokuwa wanasubiri kufutiliwa mbali kama “ndoto ya mchana” wanamkimbilia Mungu kwa toba na wongofu wa ndani; wanasali kwa kusukumwa na matumaini ya msamaha wa Mungu, kuanzia kwa Mfalme wa Ninawi aliyesema “ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuacha hasira yake kali tusiangamizwe?”. Wananchi wa Ninawi wakaona ukweli na kuokolewa na Mungu. Chini ya huruma ya Mungu pamoja na mwanga wa Fumbo la Pasaka, Fumbo la kifo linaweza kuonekana kuwa ni ”dada” kama anavyofafanua Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa kuwa ni tukio ambalo linaamsha matumaini na hatimaye, kukutana na Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.