2017-01-17 15:05:00

Yohane Mbatizaji ni mpande asiyekuwa na "noma"!


Katika mikutano rasmi kunakuwa na MC anayetambulisha mgeni rasmi. Leo tutamwona mtu atakayetutambulisha rasmi mtu tunayetakiwa kumsikiliza kwa mwaka mzima. Habari za utambulisho huo zinaletwa kwetu na mwinjili Yohane. Mwinjili huyu ndiye anayemtaja mtambulishaji wa mgeni rasmi anaposema: “Anakuja mtu aliyetumwa na Mungu, jina lake Yohane, aliyeshuhudia ule mwanga.” Kwa hiyo Yohane mbatizaji ndiye MC anayejua anachokitambulisha au kukishuhudia.

Ili kuuelewa vyema mambo yalivyojiri, tuyatathmini kwanza mazingira ya kijiografia na ya kihistoria ya utambulisho huo. Kijiografia ilikuwa ni kando ya mto Yordani. Mtambulishaji alikuwa Yohane mbatizaji. Aliyewaalika watu na kuwavusha upya katika mto Jordani na kuwaingiza katika nchi mpya ambayo siyo ya kimwili bali ya ufalme mpya wa Mungu. Kihistoria, fasuli inaanza hivi: “Siku ya pili Yohane Mbatizaji akamwona Yesu anakuja kwake.” Siku ya kwanza Yohane alikutana na wawakilishi wa makuhani na walawi, waliotumwa kwenda kwake kutoka Yerusalemu ili wamwulize, “wewe u nani?” Yohane akawajibu kifupi tu kwamba “Mimi siye Kristo, bali yuko mwingine anayefika baada yangu. Mimi sina hata hadhi ya kufungua gidamu za viatu vyake. Mambo hayo yalitokea Bethania ng’ambo yaYordani, alikokuwa Yohane akibaiza.” (Yoh. 1:19-28). Kumbe kazi ya MC ya kutambulisha ilikuwa siku ya pili. Yohane Mbatizaji alipomwona tu Yesu anakuja kwake akamwonesha kidole kama vile angemkaribisha mtu jukwaani na kusema: “Angalieni! anaingia ulingoni.” Kwa utambulisho huu kwa vile hawatajwi wasikilizaji, basi wasikilizaji hao ni sisi. “Mtazameni Mwanakondoo wa Mungu, huyu ndiye aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”

Katika utambulisho huo wasikilizaji tunaweza kuhoji maswali mawili. Swali la kwanza: Yohane anataka kusema nini anapotuonesha Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu? Kwa kawaida mtoto anabatizwa jina atakaloitwa maisha yake yote. Hapa tulimtegemea Yohane mbatizaji angemjulisha Yesu kwa jina la Masiha, Mtawala, Mtawala, Mshindi au “Simba wa Yuda.” Lakini Yohane anamtambulisha kwetu kama: “Mwanakondoo.” Jina hili mwanakondoo limetumika mara mbili katika biblia. Mosi kuhusiana na damu ya kondoo iliyopakwa milangoni mwa nyumba za wayahudi kabla ya kutoka utumwani Misri.

Damu hiyo iliwazuia Wamisri wasiingie katika nyumba za Wayahudi na kuwaua. Kwa hiyo anayetokea ulingoni siyo simba atakayeendeleza ufalme wa mabavu wa wanyama wa porini. Ulimwengu mpya ni ule ambao wanyama wote wanabadilika kuwa kondoo. Mwanakondoo ni alama ya upole na utumishi na ya kutoa maisha hadi kifo. Pili, mwanakondoo anatamkwa katika kitabu cha Isaya juu ya mtu wa ajabu, anayeongozwa kwenda machinjoni kama kondoo. Huyo kondoo anaondoa dhambi za ulimwengu wa kale wa utawala na siyo wa utumishi. Kwa hiyo Yohane anauonesha ulimwengu mpya wa watu wanaojitolea maisha yao kuwatumikia wengine kama Mwanakondoo. Kama tunavyojibiwa katika Ufunuo: “Je, watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Nao wametoka wapi? Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuayafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo.” (Ufunuo 7:14). Yaani ni wale waliounganisha maisha yao na ya Yesu wa Kalvario alikotoa damu yake hadi tone la mwisho. Mavazi meupe ni alama ya mwanga. Kwa hiyo watu hao watang’aa katika maisha yao kama Mwanakondoo.

Swali la pili: Yohane alimtambuaje Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu? Yohane anayo mitazamo miwili ya mambo. Kwa lugha ya kigiriki namna mojawapo inaitwa blepo maana yake kuangalia au kuona kitu kwa nje. Namna nyingine ya kuangalia ni emblepo maana yake kuangalia kitu kwa ndani na kuona hadi kwenye mtima. Yohane alimwangalia Yesu kwa namna zote mbili, yaani kwa nje na kuona yale kama wanayoona watu wengine, lakini pia aliangalia ndani ya Yesu, yaani kuona hadhi ya Yesu. Kadhalika kwetu sisi, mwaka huu tutaona vituko vingi sana vitakavyosimuliwa katika Injili juu ya Yesu. Lakini tunaalikwa kutafakari vituko hivyo vya Yesu na kuona hadhi halisi ya Yesu.

Tusijidhani kwamba tunamwelewa Yesu kutokana na mambo hayo ya nje tutakayoyasikia. Kufahamu hadhi ya Yesu ni vigumu sana. Mathalani, katika fasuli ya leo, tunakuta mara mbili Yohane mbatizaji anasema: “Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu kwa amaana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua;”(Yoh. 1:31). Halafu tena“Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji aliniambia: Yeye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake.”(Yoh. 1:33). Hii inaonesha kuwa hata Yohane alifanya kazi sana hadi kuitambua hadhi ya Yesu kama Mwanakondoo. Hata sisi mwaka huu wote tunaalikwa kutambua hadhi halisi ya Yesu kama Mwanakondoo anayejitoka kwa upendo na kumfuata.

Yohane, anaendelea kutoa vigezo vya hadhi ya mwanakondoo anayemtambulisha kuwa: “Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake. Tunarejezwa siku ya ubatizo wa Yesu. Neno nimemwona kwa kigiriki ni tetheamai maana yake ni kutafakari. Hapa Yohane anayo mitazamo miwili ya mambo, kwanza ule wa kawaida, halafu na ule wa hali ya juu zaidi unaotokana na kutafakari. Mtazamo huu wa pili ni wa wale walio na moyo safi. “Heri wenye moyo safi maana watamwona Mungu.” Mungu haonekani, lakini wenye moyo safi wanaweza kuona vitu visivyoonekana kwa macho ya kawaida. Kumbe ili kuona visivyoonekana, inabidi tuwe na moyo safi, mnyofu, usiyeshikamana na mambo  na miungu ya ulimwengu huu. Yohane anaona na Roho mtakatifu aliyeshuka kama hua na kubaki katika Yesu. Hua ni alama ya kudumu na ya kung’ang’ana na kiota chake. Hivyo Roho yuko katika Yesu, yaani maisha ya kimungu ambayo ni ya upendo ulio ndani yake.

Yohane mbatizaji anakiona kipengee kingine cha hadhi ya Yesu anaposema: “Huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.” Yaani, Yesu mwenyewe amejaa roho ya kimungu. Kwa hiyo, Yesu hamzamishi mtu katika maji kama alivyofanya Yohane, bali anamzamisha katika maisha, katika roho ya maisha ya kimungu aliyo nayo yeye mwenyewe. Wale wanaomfuata Yesu wanazamishwa katika roho ya kimungu, roho ya nguvu maisha ya upendo na ya kuwa mtumishi kwa wengine daima. Hadhi nyingine ya Yesu inathibitishwa na Yohane anaposema: “Wala mimi sikumjua; Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.” Yaani Yesu ni mwana wa Mungu. Mwana maana yake kufanana siyo kwa kuzaliwa kibaolojia. Kwa hiyo Yohane Mbatizaji anatutambulisha Yesu siyo tu kama Kondoo bali pia kama Mwana.

Ndugu zangu tupo mwanzoni mwa mwaka. Yatubidi daima tumkazie macho Yesu kwa sababu katika yeye tunaona mwanga wa Mungu, uso wa mtu aliyefanikiwa, anayeishi kama mwanakondoo. Katika Misa takatifu tunasiki: “Tazama mwanakondoo wa Mungu.” Katika karamu ya mwisho Yesu alichagua mkate kama alama yake, kuonesha kwamba maisha yake yote yalikuwa ni majitoleo na utumishi kwa ajili ya wengine. Tunakula mwili wa Yesu ili kufanana naye, ili tuwe kondoo katika maisha yetu katika kujitoa kwa wengine. Tuunganishe maisha yetu na yale ya Yesu aliyejitoa maisha yake kama kondoo kwa ajili ya wengine.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.