2017-01-17 14:27:00

Kanisa linawahitaji waamini jasiri, wenye matumaini na wanaothubutu!


Wakristo wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa na ujasiri unaojikita katika matumaini ili kuweza kupambana kufa na kupona na nyakati za giza na mahangaiko ya ndani, badala ya kukimbia na kujifungia katika jokofu! Kanisa haliwahitaji Wakristo waoga, watu waliosimama katika maisha yao kama “Ngongoti”, kwani waamini wa namna hii, Kanisa kwao ni kama maegesho ya magari mabovu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican sanjari na Kumbu kumbu ya Mtakatifu Anthony, Abate inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 17 Januari. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuachana na uvivu ili kuonesha ujasiri kwa kupiga moyo konde, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini ili kuleta mabadiliko katika maisha. Kwa bahati mbaya hata ndani ya Kanisa kuna waamini ambao ni wavivu kupindukia, kwao Kanisa limegeuka kuwa kama nyumba ya maegesho kwa kujihakikishia usalama, hatari kwa maisha ya kiroho!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa na ujasiri unaojikita katika matumaini, kwani waamini wazembe na wachovu, wamepoteza fadhila ya matumaini katika maisha yao, tayari wanafurahia “maisha ya pensheni ya uzeeni”. Waamini wajiandae kwenda pensheni baada ya kuchakarika kwa kazi na utume, badala ya kujikuta wanakula pensheni ya uzeeni katika maisha yao yote! Hatari kubwa! Matumaini yawasaidie waamini kupambana na maisha pasi na kukata wala kukatishwa tamaa hasa wakati wa shida na giza la maisha ya kiroho.

Ujumbe ambao Mama Kanisa anataka kuwapatia watoto wake ni kukimbilia na kuambata matumaini ambayo kamwe hayawezi kumdanga mtu, kwani hii ni fadhila inayompatia mwamini dira na mwelekeo mpana zaidi wa maisha badala ya kujifungia katika ubinafsi wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujitaabisha kuitafakari fadhila ya matumaini ili kuweza kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Waamini jasiri na wenye matumaini wakati mwingine hukosea, lakini wanapaswa kuwa na ujasiri wa kusimama na kuendelea na safari ya maisha, kwani kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu!

Bila kuthubutu, hakuna kinachoweza kutendeka anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kila mwamini anapaswa kujiuliza moyoni mwake, ikiwa kama yuko wazi au amejifungia katika ubinafsi wake; nyakati za magumu na giza la maisha, Je, yuko tayari kuambata fadhila ya matumaini hadi kieleweke kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu kwa ahadi zake. Mwishoni, Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, anawataka waamini kuchunguza kwa makini hali yao ya imani ili kweli waweze kuwa na ujasiri pamoja na matumaini ili kukabiliana na changamoto za maisha kwa moyo mkuu na thabiti. Waamini washinde kishawishi cha ubinafsi kinachooneshwa na Wakristo wachovu na wasiotaka kujibidisha na matokeo yake ni kujitafuta wao wenyewe. Wakristo wawe na ujasiri wa kuinua vichwa vyao kwa matumaini ili kutazama yale yajayo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.