2017-01-17 12:18:00

Kanisa linataka kusikiliza na kujibu kilio cha mahangaiko ya watu!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu lililoundwa na Baba Mtakatifu Francisko na kuanza kutekeleza dhamana na majukumu yake tarehe Mosi, Januari 2017 anasema, maadhimisho ya Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani yanalenga kuwapatia sauti wakimbizi na wahamiaji, wanaoteseka, wanaonyanyaswa na kutengwa. Lakini, kwa namna ya pekee, Mwaka 2017, Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwa ni sauti ya watoto wakimbizi na wahamiaji ndiyo maana kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka 2017 ilikuwa“Wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti”.

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ni muungano wa: Baraza la Kipapa la Haki na Amani; Baraza la Kipapa la Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; Baraza la Kipapa linaloratibu Misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum pamoja na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ni matunda ya mchakato wa mageuzi yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kuweza kuwa Sekretarieti ndogo inayokidhi mahitaji ya Kanisa la Kiulimwengu kwa kusoma alama za nyakati.

Baraza hili jipya litakuwa na kitengo cha tafiti; utekelezaji wa miradi; mawasiliano; mahusiano na Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali, kwa ajili ya mafao ya wengi. Kutakuwa na Idara ya Wakimbizi na Wahamiaji, changamoto inayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake! Kanisa chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko linataka kuwa karibu na mateso na mahangaiko ya binadamu, kwa kusikiliza kilio chao na kukipatia jibu kwa wakati muafaka; jibu linalofumbatwa katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu:kiroho na kimwili.

Kardinali Turkson anaendelea kusema, kuna watu wanaoendelea kufa maji na utupu huko Jangwani na Baharini kutokana na kukimbia vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; majanga asilia; dhuluma na nyanyaso hasa za kidini pamoja na kutaka kupata maisha bora zaidi. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2016 zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 5,000 wamefariki dunia wakiwa njiani kuvuka Bahari ya Mediterrania kwenda Barani Ulaya, kati yao kuna idadi kubwa ya watoto ambao wengi wao hawakuwa na wazazi wala walezi wanaosindikizana nao! Matokeo yake ni watoto hawa kupoteza maisha yao kwenye tumbo la bahari!

Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watoto 100, 000 wenye umri chini ya miaka 18 walikuwa kwenye misafara ya wakimbizi na wahamiaji bila ya kusindikizana na wazazi pamoja na walezi wao katika kipindi cha Mwaka 2015. Kardinali Turkson anasema hii ni changamoto ya kijamii inayopaswa kuvaliwa njuga na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili kuhakikisha kwamba, watoto hawa wanapatiwa ulinzi na usalama, ili wasitumbukizwe kwenye mikono ya wafanyabishara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; watu wenye uchu wa mali wanaotaka kujitajirisha hata kwa damu ya watoto wadogo! Kwao utu na heshima ya binadamu havina thamani, bali kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni fedha na mali!

Kardinali Turkson anasema, maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani ni fursa pia ya kutaka kudumisha mwelekeo chanya juu ya wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanaonekana kuwa ni kero kwa Jumuiya ya Kimataifa na kusahau kwamba, hii ni rasilimali watu na nguvu kazi; ikitumiwa vyema itasaidia mchakato wa maendeleo endelevu kwa binadamu: kiroho na kimwili. Maadhimisho haya ni muda wa kuwashukuru na kuwapongeza wadau mbali mbali wanaosimama kidete kuwatetea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika utume wake, alikazia umuhimu wa mafungamano ya kifamilia kama kiini cha kuimarisha haki msingi za watoto sanjari na kuhakikisha kwamba, watoto hawa wanapatiwa fursa ya kwenda shule, ili kujenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, ikilinganishwa na hali ya maisha ya wazazi wao. Papa Francisko anakaza kusema, watoto wasiosindikizana na wazazi pamoja na walezi wao wana hatari maradufu; kwanza kabisa ni wageni wanaolazimika kuishi mbali na nchi zao za asili; pili wametengana na wazazi wao ambao kimsingi wangepaswa kuwahudumia na kuwapatia hifadhi.

Kumbe, ulinzi na usalama kwa watoto wakimbizi na wahamiaji ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee na wadau mbali mbali ili kulinda na kudumsiha haki msingi za watoto wahamiaji na wakimbizi pamoja na kuheshimu utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kuna haki msingi za watoto wakimbizi na wahamiaji zinazobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa, kumbe, zinapaswa kukuzwa na kudumishwa na wote! Ikumbukwe kwamba, idadi ya watoto wakimbizi na wahamiaji katika kipindi cha miaka  ya hivi karibuni imeongezeka maradufu kutoka watoto 12, 360 katika kipindi cha Mwaka 2015 hadi kufikia watoto 25, 772 katika kipindi cha Mwaka 2016.

Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameguswa sana na mahangaiko, mateso na nyanyaso za watoto ndiyo maana ameamua kwa namna ya pekee kabisa kuwa ni sauti ya watoto wasiokuwa na sauti; ili kuamsha dhamiri ya watu ili waweze kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watoto: kielimu, kimaadili na kiutu. Hapa, kuna haja ya kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na nchi zile wanakotoka wakimbizi na wahamiaji ili kutafuta uwezekano wa kung’oa yale mambo yanayosababisha watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao kwa lazima.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na wadau mbali mbali kuwa na sera makini kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji; kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwapokea na kuwakirimia wageni: kwa kuheshimu utu na haki zao msingi, ili hatimaye, waweze kuingizwa katika Jamii inayowahifadhi. Kunako mwaka 1996, Canada ilikuwa ni nchi ya kwanza iliyotoa sera na mikakati makini kwa ajili ya ulinzi na usalama wa watoto wakimbizi na wahamiaji. Watoto wanapaswa kupewa nafasi ya kusoma na kutunzwa vyema kwenye familia badala ya mwelekeo wa sasa kwa Serikali nyingi wa kuwaweka watoto kwenye kambi za utambulisho ambako wanakabiliwa na hatari nyingi za maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.