2017-01-13 14:25:00

Mwanakondoo wa Mungu anayejitwika zigo la dhambi za ulimwengu!


Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba, na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nawe daima! Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa safari nzima ya ukombozi wa mwanadamu! Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu anatolewa tena Altareni kama sadaka isiyokuwa na mawaa inayompendeza Mungu. Yesu ndiye yule Mtumishi mwaminifu wa Mungu asiyekuwa na mawaa; ni mwanga wa mataifa na ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu anayekuja kutimiza mapenzi ya Baba yake wa Mbinguni!

Mwaliko unaotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni kumwambata Kristo Yesu, kwa kuchuchumia utakatifu wa maisha. Huu ni wito endelevu na changamoto isiyopitwa na wakati hata kidogo. Yohane anapenda kumkumbuka, kumshuhudia na kumuenzi Mwana Kondoo wa Mungu, kwani ushuhuda wake ni wa kweli. Tukiwa mwanzoni kabisa mwa Mwaka A wa Kanisa, Yohane anatualika kumwandalia Kristo Yesu mazingira katika akili, nyoyo na vipaumbele vyetu, ili hatimaye, kuweza kulifahamu Fumbo la Msalaba, pale Kristo atakapoteswa, kufa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Leo Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti”. Baba Mtakatifu Francisko anayaangalia mateso na mahangaiko ya watoto ambao wanajikuta wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji kutokana na sababu mbali mbali. Anataka watoto hawa walindwe na kuhudumiwa kikamilifu, ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Mwinjili Yohane anamshuhudia Kristo Yesu kwa kusema kwamba, huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Huu ni ushuhuda unaotolewa na mwanafunzi yule aliyependwa na Yesu kiasi hata cha kudiriki kufuata naye tangu mwanzo wa maisha na utume wake, hadi pale atakapoinuliwa juu ya Msalaba, ili kuwakomboa wanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Katika utambulisho huu, Yohane anapenda kutoa muhtasari wa Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!

Mwinjili Yohane anakumbuka ile siku alipokutana na Kristo Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha yake! Anakumbuka ili kushuhudia na kuendeleza mchakato wa kazi ya Ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, ili waamini waweze kuambata utakatifu wa maisha, unaoshuhudiwa katika imani tendaji! Anakumbuka jinsi ambavyo Waisraeli walivyo kombolewa kutoka utumwani Misri kwa njia ya damu ya mwanakondoo iliyokuwa imepakwa kwenye milango yao.

Yesu ni Mwanakondoo wa Mungu katika Agano Jipya. Huyu ndiye yule aliyechomwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama ya Sakramenti za Kanisa wanamozaliwa waamini kwa maji na Roho Mtakatifu na kulishwa chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, yaani, Mkate wa uzima wa milele! Ni Mwanakondoo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili aweze kujitwika ubaya na dhambi ya binadamu. Hili ni ndilo Fumbo la Msalaba linalodhihirisha hekima, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Ni Mwanakondoo wa Mungu anayewaongoza waja wake katika safari ya kwenda mbinguni! Wale wote watakaobahatika kufua mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, watastahilishwa kuitwa, wateule wa Mungu, yaani watakatifu. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili hii, inatoa kwa muhtasari kabisa Imani ya Kanisa inayofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Huu ni utimilifu wa Agano la Kale na Unabii wote. Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayetaka kumwokoa mwanadamu anayejitambua kuwa ni mdhambi na hivyo anahitaji toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kutembelea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Mama Kanisa anatumbusha kwamba, daima tunazungukwa na dhambi pamoja na nafasi zake: kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na wakati mwingine kwa kutotimiza wajibu wetu. Ndiyo maana, mwanzoni mwa Ibada ya Misa Takatifu, waamini wanaalikwa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka yaani: Ibada ya Misa Takatifu. Mtakatifu Inyasi wa Antiokia anasema kwamba ni Yesu Kristo peke yake, ndiye tabibu wa kweli, anayeweza kumwondolea mwanadamu dhambi zake na kumwonjesha huruma na upendo wa Baba wa milele kiasi hata cha kuweza kuitwa mwana mteule wa Mungu. 

Tumwombe, Mwenyezi Mungu katika Juma hili, tuweze kumtambua na kumfuasa Kristo, Mwanakondoo wa Mungu, kwa kumshuhudia kwa njia ya utakatifu wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji! Tuadhimishe Mafumbo ya Kanisa kwa moyo wa: Toba, Ibada na Uchaji wa Mungu kwani katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anajitoa tena sadaka kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za ulimwengu. Tuendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa watoto wanaoteseka kama wakimbizi na wahamiaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.