2017-01-13 08:37:00

Mmewekwa kuwa ni nuru ya mataifa!


Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika kitabu chake kiitwacho The Meaning of Christian Brotherhood ametufafanulia vema juu ya udugu wa kikristo katika maana ya ndani kabisa na katika mapana yake. Yeye anasema: “Kama misingi ya Kanisa ambayo hudhihirisha utume wa Kristo imetengeneza mgawanyiko kati ya watu – yaani Kanisa na lisilo Kanisa – hivyo ni dhahiri kwamba lengo halisi ya kazi za Kristo zilielekezwa si kwa sehemu tu bali kwa kitu kizima – ilielekezwa kwa ubinadamu wote. Uponyaji wa sehemu nzima hufanyika , kadiri ya mapenzi ya Mungu, katika ulinganisho kinzani wa wengi na wachache, ambao kwao wachache huwa ni sehemu anayokusudia Mungu kuanzia ili kuokoa wengi”.

Mang’amuzi haya ya kibaba yanaunganika vema kabisa na mawazo ya Dominika hii ya pili ya Mwaka ambapo tunapewa wito wa kwenda kuwa sababu ya auheni kwa mwanadamu aliyegaragazwa na kuchakazwa kwa dhambi. Ni wito ambao unatupeleka katika ulimwengu mzima, yaani kuuganga ubinadamu wote na si sehemu tu ya ubinadamu kwani sote tu ndugu. Utume wetu kama wanakanisa si wa kugusa sehemu tu ya ubinadamu au kundi fulani tu linalorandana nasi bali ni ubinadamu wote. Undugu wa kikristo hutimiza wajibu wake kwa wote kupitia shughuli za kimisionari, agape na kujitoa bila kujibakiza kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.

Wito huo unajitokeza katika somo la kwanza ambapo Bwana anaita akisema: “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa”. Wito huu kwa taifa la Israeli unajifunua zaidi katika Kanisa zima leo. Sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu inatuonesha pedagogia mahususi ya kimungu ambaye anaanza kuimarisha kundi ndogo ili baadaye kwenda kuwa kwa ajili ya wote. Mungu anamweka huyo mtumishi wake kwanza kwa ajili ya “kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa”. Nia yake ni kuimarisha kwanza kundi dogo kwa kuisimika misingi yake kusudi baadaye liwe kielelezo kwa wengine. Mungu anasema: “zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia”.

Taswira hiyo ya Kanisa inajifunua katika Kristo ambaye Yohane Mbatizaji anamshuhudia kwamba ni Mwana Kondoo wa Mungu azichukuaye dhambi za ulimwengu. Dominika iliyopita tulimpambanua kama Mwana mpendwa na mteule wa Mungu ambaye Roho wa Mungu yu juu yake. Haiba hii ndiyo inayomstahilisha kuutimiza huo utume wake ulio utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa mwanadamu tangu mwanzo wa historia ya wokovu wetu aliposema: “nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake” (Mw 3:15).

Kristo aliye kichwa cha Kanisa anatambulishwa kama yeye anayekuja kuiondoa dhambi ya ulimwengu, dhambi ambayo ilimtenga mwanadamu na Mungu muumba wake, ikamfanya kuwa mwana mkiwa anayeangaika na kutangatanga huku na kule na kutafuta faraja. Dhambi hiyo ya ulimwengu ilimfukuzisha mwanadamu kutoka katika bustani ya Edeni na kushindwa kuyafaidi matunda yake, kujifariji chini ya kivuli chake na kuufurahia upepo wake mwanana. Huyu ni mwanadamu anayemtenga mwenyezi Mungu na shughuli zake za kila siku na kwenda kutafuta faraja katika viumbe vyenye ukomo na vyenye kutoa ahadi isiyodumu.

Hali hii inamwacha mwanadamu kuwa katika hali ya uchovu na kuchakaa kabisa. Ni hali ambayo tunaishuhudia leo hii katika jamii yetu ya kibinadamu. Dhambi ya ulimwengu inamtenga mwanadamu na Mungu. Kristo anatambulishwa kama Mwanakondoo wa Mungu, utambulisho ambao unatudokezea fumbo la Pasaka ambalo kwalo anazichukua dhambi zetu zote na kuzigongomelea pale juu Msalabani, ishara ya utii wa juu kabisa katika kuyatimiza  mapenzi ya Mungu. Hii ni kwa sababu njia hii ya utii unaoleta wokovu inakinzana na kiburi au ukaidi wa mwanadamu ambao ulimwingiza katika dhambi. Ni katika utii huo mithili ya Kristo mwanadamu ataweza kujiondoa katika utumwa wa dhambi na kuwa tena mwana huru wa Mungu.

Mwenyezi Mungu amesema kwamba ataweka uadui kati ya shetani na mwanadamu. Kusudi lake ni kumtenganisha mwandamu na shetani na hila zake zote kwani mwanadamu anapoendelea kung’ang’ana kwa shetani matokeo yake hujitenga na Mungu muumba wake na hivyo kuishia katika maisha ya mashaka, hofu na mahangaiko. Hivyo, Kristo, Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu anatupatia utume huo na kwa maneno ya Nabii Isaya kutuweka kuwa nuru ya mataifa. Tunapokuwa mwanzoni kabisa mwa kipindi cha kawaida cha Mwaka wa kiliturujia wa Kanisa hatuna budi kulielewa hilo na kulifanya kuwa dira ya utume wetu.

Utume wa Mungu kwa Kanisa, hususani Kanisa ambalo sisi wabatizwa ni kuwa nuru ya mataifa. Mwenyezi Mungu ametuchagua, akatuandaa na kutushushia Roho Mtakatifu kusudi twende kuwa nuru kwa wengine. Wimbo wa Zaburi unatualika kuitikia tukisema “Tazama nimekuja, kuyafanya mapenzi yako”. Tuitikie kwa ujasiri na moyo wa matumaini kwani Yeye anayetuita ndiye mwenyewe atakayetutia nguvu na kutuwezesha. Hivyo jukumu letu ni kuyatafakari mapenzi yake na kuyatekeleza huku tukiwezeshwa na neema na amani zitokazo kwake na kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Leo hii sisi wana Kanisa ambao tumekwishaianza safari yetu ya maisha katika ulimwengu wetu tutembee na wazo hilo kwani Mkristo anapaswa kuwa ni ahueni kwa mwanadamu aliyechakazwa na giza la dhambi na pia amewekwa ili kwenda kuwa nuru kwa dunia yote.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.