2017-01-12 14:53:00

Maaskofu Kenya wasema: Serikali na wapinzani wajadiliane!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limeitaka Serikali iliyoko madarakani pamoja na vyama vya upinzani kuhakikisha kwamba wanakumbatia na kuambata majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na demokrasia nchini humo. Wito wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya unafuatia hatua ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kutia mkwaju kwenye Muswada wa Mabadiliko ya Sheria za Uchaguzi wa Mwaka 2016, ambao kwa sasa umekuwa ni sheria licha ya upinzani uliotolewa na vyama vya upinzani pamoja na wadau mbali mbali za demokrasia nchini Kenya.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa mkwaju na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya na kuwasilishwa na Askofu Philip Anyolo, Maaskofu Katoliki wanasema, bado kuna nafasi ya kufanya mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kufikia maridhiano kati ya Serikali na Vyama vya upinzani. Viongozi wakuu wa dini mbali mbali nchini Kenya wako tayari kusaidia mchakato huu wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kweli uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Kenya kwa Mwaka 2017 unakuwa huru na wa haki.

Mchakato mzima wa uchaguzi mkuu nchini Kenya unapaswa kujikita katika ukweli, uwazi, haki na amani; daima ustawi na maendeleo ya Wakenya wote vikipewa msukumo wa kwanza. Kuna kinzani, migogoro na mipasuko ya kisiasa inayoendelea kusababaisha giza katika masuala ya kisiasa nchini Kenya; jambo ambalo linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kujikita katika majadiliano ya kisiasa yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; ustawi na maendeleo ya wengi. Migomo, vurugu na malumbano yasiyokuwa na tija wala maendeleo kwa wananchi wengi wa Kenya hayafai kwa wakati huu na badala yake, mchakato wa majadiliano unapaswa kuanzishwa mara moja ingawa Maaskofu wanatambua haki ya wananchi kuandamana au kugoma kadiri ya Katiba ya nchi! Katika hali kama hizi, mara nyingi watu wamepoteza maisha na mali zao, kiasi hata cha kuhatarisha umoja na mafungamano ya kitaifa!

Wakati huo huo, tarehe 11 Januari 2016 viongozi wa Upinzani Bwana Musalia Mudavadi wa A.N.C, Bwana Kalonzo Musyoka wa Chama cha Wiper Movement, Mkongwe wa upinzani Bwana Raila Odinga wa Chama cha ODM, Bwana Moses Wetangila wa Chama cha Ford Kenya pamoja na Bwana Nick Salat wa Chama cha KANU wameamua kuunganisha nguvu zao, ili kupambana na Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto kutoka Chama cha Muungano wa Jubilei wakati wa kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu nchini Kenya unaotarajiwa kufanyika mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.