2017-01-12 14:21:00

Maaskofu Katoliki Italia: Onesheni ukarimu kwa wakimbizi!


Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, katika maadhimisho ya Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2017 yanayoongozwa na kauli mbiu “Wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti”, Kanisa Katoliki nchini Italia linaunga mkono mchakato wa ukarimu na upendo kwa wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Linapinga kwa nguvu zote mchakato wa kujenga tena vituo vya utambulisho wa wakimbizi na wahamiaji nchini Italia.

Ukarimu na upendo huu unapaswa kuwa makini kwa kuzingatia tofauti na historia ya kila mtu! Maaskofu wanaunga mkono jitihada za kuwaingiza watoto wahamiaji na wakimbizi wasiokuwa na wazazi wala walezi wao katika familia badala ya kuwajengea vituo vya watoto yatima. Serikali ya Italia iangalie uwezekano wa kutunga sheria inayowapatia uraia  wanafunzi wakimbizi na wahamiaji waliohitimu shule ya msingi nchini Italia.

Askofu Nunzio Galantino anasema, haya ni mambo msingi ambayo Baraza la Maaskofu Katoliki linapenda kukazia kama sehemu ya mchango wake kwa maadhimisho ya Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 15 Januari 2017. Kanisa linapenda kuunga mkono sera na mikakati endelevu kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji nchini Italia. Kanisa pia litasimama kidete kupinga sheria, taratibu na kanuni zinazotaka kuwabeza na kuwabagua wakimbizi na wahamiaji.

Huu ni mwelekeo mpya wa kuthamini mchango unaotolewa na Serikali katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaohifadhiwa nchini Italia kwenye vituo vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Serikali, bila kusahau ukarimu na upendo wa familia mbali mbali nchini Italia ambazo zinatoa hifadhi kwa watoto wakimbizi na wahamiaji wapatao mia tano. Kumbe, kuna uwezekano kabisa wa kusaidia kutoa hifadhi kwa watoto wakimbizi na wahamiaji; kwa kuzingatia elimu makini na mafungamano ya kijamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linapinga mchakato wa kufungua tena Vituo vya Kuhakiki Utambulisho wa Wakimbizi na Wahamiaji ili kuwafukuza wale wote watakaokosa sifa ya kuwa wakimbizi au wahamiaji nchini Italia. Baraza la Maaskofu linapinga mchakato huu kwani vituo hivi vimekuwa ni kielelezo cha mateso, nyanyaso na suluba kubwa kwa wakimbizi na wahamiaji, kiasi cha kuonekana kuwa kama ni magereza ya wakimbizi. Vituo hivi vinaweza kusababisha kushamiri kwa mchakato wa kuunda watu wenye siasa na misimamo mikali ya kidini na kiimani, hatari sana katika amani na usalama wa nchi.

Kwa upande wake, Monsinyo Guerino Di Tora, Rais waTume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia inayoshughulikia wahamiaji na wakimbizi pamoja na Mfuko wa Wakimbizi “Fondazione Migrantes” anasema watoto wakimbizi na wahamiaji ni nguvu na matumaini ya Jamii katika ujumla wake. Hawa ni watoto ambao wanachangamotishwa kujenga na kukuza utu na heshima ya binadamu; haki na amani. Monsinyo Gian Carlo Perego, Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Wakimbizi nchini Italia anasema, kuna haja ya kuibua na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kitamaduni sanjari na kutambua uraia unaothamini na kujali kizazi hiki kipya cha wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi nchini Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.