2017-01-10 10:55:00

Maaskofu kuendelea kuratibu mchakato wa upatanisho DRC


Rais Joseph Kabila wa DRC ameamua kwa dhati kabisa kulikabidhi Baraza la Maaskofu Katoliki DRC dhamana ya kuendelea kuwa ni chombo cha upatanisho wa kitaifa hadi pale uchaguzi mkuu utakapofanyika mwishoni mwa Mwaka 2017 kadiri ya makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Serikali na Vyama vya upinzani nchini DRC. Rais Kabila anasema, atajitahidi kutekeleza kwa dhati makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Vyama vya upinzani baada ya Rais Kabila kuwa amehitimisha rasmi muda wake wa Kikatiba wa kukaa madarakani hapo tarehe 20 Desemba 2016.

Kutokana na makubaliano hayo, Rais Kabila ataendelea kuwepo madarakani kwa muda wa Mwaka mmoja na atapaswa kuteuwa Waziri mkuu kutoka katika Vyama vya upinzani, ili kwa pamoja waweze kusimamia na kuendeleza mchakato wa uchaguzi mkuu nchini DRC pamoja na kuundwa kwa Baraza la Kitaifa ambalo litakuwa chini ya usimamizi wa  Bwana Etienne Tshisekedi, mmoja wa wapinzani wakongwe nchini DRC. Mwezi Machi, 2017, Bunge litajadili na kupitisha muswada wa sheria unaounda Baraza la Kitaifa.

Rais Joseph Kabila kwa upande wake, ameonesha nia ya kutokuwania tena awamu ya tatu ya Urais nchini DRC, hali ambayo ingezua tena machafuko ya kisiasa kama ilivyojitokeza katika nchi jirani ya Burundi na Rwanda. Makubaliano haya ya kisiasa ni juhudi za Baraza la Maaskofu Katoliki DRC katika kipindi cha mwezi mzima, chini ya usimamizi wa  Askofu mkuu Marcel Utembi Tapa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC. Changamoto kubwa mbele yao kwa sasa ni kupanga tarehe rasmi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2017 pamoja na kuvishirikisha vyama vingine vya upinzani ambavyo havikuwemo kwenye orodha ya kwanza. Muundo wa Baraza la Kitaifa na orodha ya mawaziri wanaopaswa kuteuliwa ni changamoto inayoendelea kufanyiwa kazi nchini DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.