2017-01-10 10:18:00

Huruma na msamaha ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa amani!


Balozi Armindo Fernandes do Espirito Santo Vieira, Dekano wa Mabalozi wanaowakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, kutoka nchini Angola, Jumatatu, tarehe 9 Januari 2017 kwa niaba ya Mabalozi wenzake, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kupembua kwa kina na mapana dhana ya huruma ya Mungu wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii inaonesha kwamba, msamaha ni njia muafaka katika kukuza na kudumisha mchakato wa upatanisho. Kimsingi huruma ni dhana inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu na kamwe si jambo linaloelea kwenye ombwe!

Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko katika juhudi zake za kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, kama chachu ya ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu! Hii ni changamoto kwa dini mbali mbali duniani kuhakikisha kwamba, zinakuwa kweli ni chachu na mhimili mkuu wa ujenzi wa haki, amani na upendo duniani. Balozi Armindo Fernandes do Espirito Santo Vieira anakaza kusema, uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni tukio ambalo limedhihirisha kwamba, majadiliano ya kiekumene ni jambo ambalo linapaswa kusonga mbele kama ilivyojitokeza hata kwa Makanisa mengine ya Kikristo kwa kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Makanisa haya.

Huu ni umoja na mshikamano wa Makanisa kama kielelezo cha ushuhuda wa kumtangaza Kristo Yesu kwa njia ya huduma makini kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji sanjari na kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni chombo na shuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mataifa. Ukweli na uwazi; upendo na mshikamano unaooneshwa na Baba Mtakatifu ni kielelezo kwamba, kinzani na mipasuko ya kijamii inaweza kupatia ufumbuzi wake, ili kukuza na kudumisha haki na amani duniani.

Balozi Armindo Fernandes do Espirito Santo Veira anasikitika kusema, licha ya juhudi za kutaka kukuza na kujenga amani dunia, lakini bado kuna vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kupandikiza mbegu ya hofu na kifo sehemu mbali mbali za dunia. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii bado inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao huko Afghanstan, Iraq, Libia, DRC, Yemen, Siria na Sudan ya Kusini. Haya ni maeneo ambayo mchakato wa kutafuta amani na usalama bado una safari ndefu ya kufanya! Imekuwa ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea wafanyakazi wa Jumuiya ya Kimataifa waliopoteza maisha yao wakati wakitekeleza dhamana na wajibu wao kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Pamoja na changamoto zote hizi, Jumuiya ya Kimataifa haina sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa kwani amani ni tunu ya thamani kubwa kwa watu wote, ili kukuza na kudumisha maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa, kuhakikisha kwamba, inadhibiti na kumaliza vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ambayo inachangia kwa sehemu kubwa kuzalisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.