2017-01-08 14:30:00

Mshikamano wa Papa Francisko kwa maskini wanaokufa kwa baridi na utupu


Kutokana na kushuka kwa joto sehemu mbali mbali za Italia, tayari kuna watu kadhaa ambao wamefariki dunia kutokana na utupu pamoja na baridi kali, wengi wao ni maskini na wale wasiokuwa na makazi maalum! Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso ya watu wasiokua na makazi maalum kuzunguka eneo la Vatican, ameamuru kwamba, nyumba zinazotoa huduma kwa maskini mjini Vatican, ziwe wazi kwa muda wa masaa 24 ili kuokoa maisha ya maskini watakaokuwa wanahitaji hifadhi. Hata kama hakuna mahali pa kuwalaza, walau wapewe mahali pa kujihifadhi na chakula cha moto!

Hayo yamesemwa na Askofu Konrad Krajewski, Mtunza sadaka  mkuu wa Vatican ambaye amekazia kwamba, Nyumba ya “Dono di Maria” “Zawadi ya Maria” inayohudumiwa na Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Masista wa Mama Theresa wa Calcutta na nyumba ya “Dono di Misericordia” “Zawadi ya “huruma ya Mungu” iliyofunguliwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma Mungu zitakuwa wazi kutoa huduma ya dharura kwa maskini na wahitaji. Kwa wale ambao wataridhia kuendelea kukaa katika maeneo yao ya kila siku, Vatican imeamua kuwapatia mablanketi ya baridi pamoja kuwahifadhi kwenye magari maalum.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, walau hakuna mtu anayefariki dunia kwa baridi na utupu kutokana na umaskini wake, kuzunguka maeneo ya Vatican. Huduma inayotolewa na Idara ya Sadaka ya Kitume ni fedha ambayo imekusanywa kutoka kwa wasamaria wema na wale wanaohitaji baraka za kitume kutoka Vatican. Vikosi vya ulinzi na usalama vya Vatican navyo vinashiriki kikamilifu katika mchakato unaaopania kuokoa maisha ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum kuzunguka Vatican, kwani Kanisa linatambua kwamba, maskini ni amana na hazina ya Kanisa, wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.