2017-01-07 12:30:00

Mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana!


Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni kati ya changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwanza kabisa kwa kuheshimu utu na haki zao msingi, kwani hata wao pia wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 103 ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2017 unaongozwa na kauli mbiu “Wahamiaji wadogo ni wahanga wasiokuwa na sauti”. Siku hii inaadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 15 Januari 2017.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kuanzia Jumapili, tarehe 8-14 Januari 2017 linaadhimisha Juma la Wakimbizi na Wahamiaji nchini Marekani. Lengo la maadhimisho haya ni kusaidia kuwaelimisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhusu matatizo, changamoto na fursa zinazopatikana kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nchini Marekani. Maadhimisho ya Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Kujenga utamaduni wa watu kukutana”.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba,  kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2015 kumekuwepo na ongezeko kubwa la wakimbizi kutoka milioni 15.9 hadi kufikia milioni 21.3. Idadi ya wahamiaji katika kipindi hicho imeongezeka kutoka wahamiaji milioni 172.7 hadi kufikia wahamiaji milioni 243.7 kwa mwaka 2015. Haki msingi za wakimbizi na wahamiaji zisiposimamiwa kidete, wengi wao watajikuta wakitumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mambo ambayo kimsingi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kuna zaidi ya watu milioni 65 wanaolazimika kuzikimbia au kuzihama nchi zao, idadi ambayo inaendelea kuongeza maradufu kila kukicha, kiasi cha kulifanya wimbi la wakimbizi na wahamiaji kuwa ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limeamua kuadhimisha Juma la Wakimbizi na Wahamiaji, ili kuwasaidia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutambua sababu, matatizo, changamoto na fursa ambazo zinaweza kupatikana kwa kuwakaribisha na kuwaingiza katika mfumo wa maisha ya jamii husika.

Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto endelevu na wala si tatizo mtambuka! Ni dhana ambayo imejikita katika utamaduni na Mapokeo ya Kanisa tangu Agano la Kale. Askofu Joe Vàsquez wa Jimbo Katoliki la Austin, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wahamiaji Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani anasema, maadhimisho ya Juma la wakimbizi na wahamiaji ni fursa ya kuwaonesha watu hawa: huruma na upendo; haki na mshikamano wa dhati, kwani wao pia ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hiki ni kipindi cha kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema namna ya kuchangia katika kuwaenzi wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi nchini Marekani. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika maadhimisho haya kwa Mwaka 2017 linasherehekea Jubilei ya Miaka 25 tangu maadhimisho haya yalipoanzishwa na Kanisa Katoliki nchini Marekani. Tangu wakati huo, Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuhakikisha kwamba, haki zao msingi zinalindwa na kuheshimiwa na wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.