2017-01-07 12:06:00

Jubilei ya miaka 50 ya huduma ya upendo na mshikamano!


Familia ya Mungu nchini Canada inaendelea na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Canada, ambalo limekuwa ni “jembe” la nguvu katika mchakato wa kukuza na kudumisha maendeleo endelevu sanjari na kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, amani, ustawi na maridhiano kati ya watu! Caritas Canada ilianzishwa kunako mwaka 1967 ili kuwasaidia maskini, waliokuwa wananyanyasika na kudhulumiwa haki zao msingi pamoja na kuwasaidia wananchi wa Canada kujenga moyo wa upendo na mshikamano na maskini sehemu mbali mbali za dunia, kama ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Kilele cha Jubilei ya Caritas Canada ni mwaka 2017.

Hii ni changamoto endelevu hata baada ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Caritas Canada. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika barua yake kwa ajili ya maadhimisho haya linasema, Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa ya kutafakari kwa kina mihimili ya imani ya Kanisa, yaani, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka na umuhimu wa kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni kielelezo makini cha Uinjilishaji mpya, unaowasukuma waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na huruma miongoni mwa watu wa Mungu.

Maaskofu wanatambua kwamba, wamepewa dhamana na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanafundisha, wanaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani! Lakini, Caritas Canada, imekuwa mstari wa mbele katika kuwashirikisha watu Injili ya imani na matumaini ya Kikristo, kwa kutambua kwamba, haki, amani na huruma ni chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Caritas Canada, limekuwa ni “jembe” la nguvu katika huduma za maendeleo kwa familia ya Mungu inayoogelea katika dimbwi la umaskini, ujinga na njaa.

Msaada wa hali na mali, umesaidia kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na maendeleo ya watu waliobahatika kunufaika na msaada huo sehemu mbali mbali za dunia kama vile Haiti na Ufilippini walioathirika kwa kiasi kikubwa na majanga asilia katika miaka ya hivi karibuni. Huu ni msaada unajikita katika huduma ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Caritas Canada imekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji huko Mashariki ya Kati hususan nchini Syria ambako watu wanaendelea kupoteza maisha kutokana na vita isiyokuwa na kichwa wala miguu!

Caritas imekuwa pia mstari wa mbele katika kuragibisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya haki, amani na mshikamano wa kweli bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Lengo la Caritas Canada ni maendeleo ya mtu mzima kiroho na kimwili, ili kuinua utu na heshima yake tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya maisha yake. Ni maendeleo yanayopania kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli familia ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya huruma, upendo na mshikamano, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na maisha, dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine.

Waamini walei wanapaswa kuendelea kushikamana na kushirikiana na viongozi wa Kanisa katika mchakato wa kupambana na changamoto za maisha ya mwanadamu, ili kweli haki, amani na mshikamano viweze kutawala akili na nyoyo za watu! Ushirikano huu usaidie kupambana na umaskini, baa la njaa, ujinga na magonjwa mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; tayari kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaofariji; unaoganga na kuponya majereha ya watu waliokata tamaa kwa mafuta ya huruma na divai ya upendo.

Ikumbukwe kwamba, waamini walei wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao! Maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kufumbatwa katika Injili ya upendo kama alivyokazia Mwenyeheri Paulo VI na Baba Mtakatifu Francisko. Pasi na Injili ya huruma na upendo, utu na heshima ya binadamu viko mashakani. Huruma na upendo ni mihimili mikuu ya imani kwa Kristo na Kanisa lake. Mshikamano na utekelezaji wa haki jamii ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa.

Familia ya Mungu nchini Canada, itaendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya furaha, amani, upendo na mshikamano pamoja na kuendelea kuwajengea vijana uwezo wa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Jubilei ya miaka 50 ya Caritas Canada ni muda muafaka wa kujizatiti katika utambulisho wa umoja, utume na dhamana ya Kanisa katika huduma ya upendo. Hivyo ndivyo Askofu Douglas Crosby, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, anavyohitimisha barua yake ya kichungaji kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Caritas Canada yanayofikia kilele chake mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.