2017-01-06 14:35:00

Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana: Mshikamano na binadamu mdhambi!


Katika Dominika ya Ubatizo wa Bwana watu wengi hujiuliza kwa nini Yesu alibatizwa. Je, Yeye alihitaji kufanya toba? Au Je, yeye alizaliwa na dhambi ya asili? Kwanza ni muhimu kutofautisha Ubatizo wa Yohane na ubatizo tunaopokea sisi Wakristo. Yohane Mbatizaji mwenyewe anadokeza tofauti zao akisema: “kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Mt 3:11). Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba lakini ubatizo uliosimikwa na Kristo unatufanya kuwa wafuasi wake. Ubatizo unaoanzishwa na Kristo unatufanya kuwa watoto wa Mungu, unatuunganisha naye na hivyo kutuondolea laana ya milele iliyoletwa na dhambi ya asili.

Ili kuelewa sababu za Yesu kubatizwa ni vema kuyasoma mazingira ya ubatizo wake. Baada ya kuzaliwa kwake na kisha kutolewa hekaluni tunamsikia Kristo mara moja tu katika maisha ya hadharani wakati akiwa na umri wa miaka kumi na miwili. Baada ya hapo ameendelea na maisha ya ufichoni hadi kipindi hiki anapojitokeza na kutaka kuanza rasmi utume wake. Hivyo tukio hili lilitokea wakati akijitambulisha kwa watu wake. Tendo la ubatizo wake ni kuonesha mshikamano na watu wake ambao kama mwandishi wa Waraka kwa Waebrania anasema: “Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake” (Ebr 2:11). Kristo amejifananisha na watu wake tangu mwanzo, amekuwa sawa na sisi wanadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Hivyo ubatizo wake ulilenga zaidi katika kumtambulisha Yeye kati yetu na kumpatia fursa ya kuuanza vema utume wake.

Dominika ya Ubatizo wa Bwana ni mithili ya bawaba kwa sababu huyaunganisha majira mawili ya mwaka wa kiliturujia wa Kanisa, yaani katika Dominika hii tunahitimisha majira ya Noeli na hapo hapo tunaanza Majira ya kawaida ya mwaka wa Kanisa. Muunganiko huu si jambo la bahati mbaya tu bali ni mwaliko kwetu kuingia katika kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa, yaani katika maisha ya kawaida tukiwa tumejazwa chachu ya kipindi cha Noeli ambacho kimetukumbusha tena jinsi hadhi yetu kama wanadamu ilivyoinuliwa kwa fumbo la umwilisho. Kristo anapokuwa tayari kuanza utume wake katika jamii ya mwanadamu Neno la Mungu linatufunulia madhumuni na lengo la utume huo, yaani kumtumikia Mwanadamu katika ukweli na haki ili kumkomboa na kumrejeshea tena hadhi yake. Utume wake haukulenga katika kuwadidimiza binadamu katika udhaifu wao bali kuwarudishia nguvu na matumaini.

Nabii Isaya anamtaja kama mtumishi wa Mungu ambaye “mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli”. Nabii Isaya anaendelea kumwelezea kwa kumtaja kama Yeye aliyejazwa Roho wa Mungu: “Ambaye nimetia roho yangu juu yake”. Hapa tunaunganishwa na Kristo ambaye kwa hakika unabii huu ulikuwa unamuagua. Maneno haya yanajirudia pia katika sauti kutoka mbinguni kama tunavyosikia katika Somo la Injili ikisema “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye”. Kristo aliendelea kujifunua mwenyewe kwamba amejazwa na Roho wa Mungu kwa ajili ya utume kwa ukombozi wa Wanadamu: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa” (Lk 4:18 – 19)

Kristo ambaye tunahitimisha majira haya ya Sherehe za kuzaliwa kwake amekuwa akielezewa kabla ya majira haya wakati wa kipindi cha Majilio na hata wakati huu wa Noeli kuwa ni Maisha Mkombozi wa wanadamu. Sifa nne muhimu zinazojionesha kwake zinapaswa kutupiwa tena jicho ili kuona umuhimu wake katika utume wake ambao pia unapaswa kuwa ni utume wa Kanisa, yaani, kuutafakari ubinadamu uliochakaa; kupyaisha tena utu wa mtu. Kwanza ni kutegemezwa na Mungu yaani kumfanya Mungu kuwa chanzo na ghala la kuyachota yote yanayotakiwa katika utume. Pili ni kuwa mteule wa Mungu, yaani kule kuwa imekusudiwa na Mungu kutekeleza jukumu hilo. Hapa ni kuisikiliza sauti ya Mungu inayokuita ili kukutuma. Tatu ni kuwa mpendwa wa Mungu. Wakati wa uumbaji Mungu aliumba vyote akaviona kuwa vimekuwa vizuri. Ukamilifu wetu katika ukweli ndiyo unatufanya kuwa wazuri na hivyo kupendeka kwa Mungu. Na nne ni kuwa umejazwa na Roho wa Mungu. Huyu ni Roho Mtakatifu ambaye Kristo anatuambia atakapokuja kwenu “atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia (Yoh 14:26), “atanishuhudia” (Yoh 15:26), “atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari” (Yoh 16:13).

Hivyo, Dominika hii inapotuingiza katika kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa tunapaswa kuongozwa na mambo hayo manne kwa ajili ya kufanya utumishi wenye tija. Utume wetu unapaswa kutendwa kufuatana na maongozi ya Mungu. Tunapokuwa wana wapendwa wa Mungu tunapaswa kutembea katika ukweli na kutenda haki. Maisha ya mwanadamu yanapokuwa  katika ukweli na haki huondoa upendeleo na hisia binafsi. Mtume Petro analionesha hilo akiwa Yafa kwa kusema “hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa naye”.Kuwa mwana mpendwa wa Mungu na hivyo kubaliwa naye kunakudai kujinasua katika kongwa la kufuata matamanio na maongozi ya kimwili au ya kidunia. Anayekubaliwa na Mungu na hivyo kutenda kadiri ya neno lake ni yule “amchaye na kutenda haki”. Kristo anapoanza utume wake anatajwa kama Mwana mpendwa wa Mungu. Hii inamaanisha kwamba utume wake unadhihirisha hiyo hali ya kutembea katika ukweli na kutenda haki bila upendeleo wowote.

Huria za kimaadili na uhuru bandia wa mwanadamu unamuondoa katika kutenda kwa haki na ukweli na matokeo yake changamoto mbalimbali za kiutu na kimaadili tunazokumbana nazo katika jamii ya wanadamu. Hali hizi humsukuma mwanadamu kujali zaidi kile kinachofurahisha nafsi yake, kile ambacho kinaipendeza roho yake hata kama kinapingana na haki na ukweli. Hakuna tena nafasi ya sifa nje ya hizo tulizoziona hapo juu. Badala ya kutegemezwa na Mungu mwanadamu anakuwa ndiye chanzo na hakimu wa matendo yake, badala ya kuisikilza sauti ya Mungu katika wito fulani kadiri ya mipango yake, mwanadamu anatenda wajibu wake kwa jinsi anavyojisikia yeye; badala ya kuwa katika uhalisia au ukamilifu kadiri ya mipango ya Mungu, mwanadamu anajitengenezea namna zake ambazo huziona zinampendeza; badala ya kuongozwa na Roho wa Mungu, yeye huisikiliza sauti ya ulimwengu na miondoko yake.

Hii ndiyo changamoto iliyopo mbele yetu tunapoingia katika kipindi hiki cha kawaida cha mwaka. Majira ya Noeli yametualika na kutuamshia tena ile hali ya thamani ambayo imesimikwa ndani mwetu kwa fumbo la umwilisho. Kristo alipotwaa ubinadamu wetu na kuwa kama sisi alilenga katika kututhibitishia sisi wanadamu uthamani uliokuwepo ndani mwetu tangu uumbaji. Mtume Paulo anatuonesha hali hiyo anaposema “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo” (Ef 1:3 – 4). Na hivyo tunarejeshewa tena uthamani huo ambao unapaswa kujidhihirisha mbele ya wanadamu kwa maisha ya upendo, amani, umoja na uelewano.

Sisi wakristo tunaishi katika jamii ambayo haioni tena thamani ya mwanadamu na inaendelea kuukandamiza utu wake. Mtumishi wa Mungu anayejifunua katika nafsi ya Kristo anakuwa kinyume na mienendo hiyo ya kidunia kwani “mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima”. Huo ndiyo utume wetu, utume wa kuwarejeshea tena matumaini wale waliokata tamaa; kuwapatia tena upendo wale wanaoteswa na manyanyaso ya kidunia; kuwafungulia wote waliofungwa na ulevi, uzinzi na uasherati; na kuwatangazia ujio wa Mungu. Wimbo wa Zaburi umetuambia kwamba “Bwana atawabariki watu wake kwa amani”. Amani hiyo ya Bwana inategemewa kububujika kutoka ndani ya kila mwanadamu. Hivyo tuingie katika majira haya ya kawaida ya mwaka wa Kanisa kwa bashasha huku tukiifunua hadhi hiyo iliyojificha ndani mwetu ya kuitwa wana wapendwa wa Mungu kwa kutembea katika ukweli na kutenda haki.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha. 








All the contents on this site are copyrighted ©.