2017-01-05 16:24:00

Watawa msijenge kuta za utengano mtazimika kama kibatari!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuanzia tarehe 3- 5 Januari 2017 limeendesha kongamano la kitaifa kuhusu miito, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Simama! Ondoka! Usiogope. Miito na Utakatifu: Mimi ni utume”. Kilele cha kongamano hili imekuwa ni fursa kwa wajumbe kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 5 Januari 2017 kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican na baadaye kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kongamano hili ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana, imani na mang’amuzi ya miito itakayoadhimishwa kunako mwaka 2018 kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa kutangaza na kushudia Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Wajumbe wamekumbushwa kwamba, Kristo Yesu anawaita na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Injili ya miito; kwa kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya ndoto za maisha, nguvu na mapungufu yao ya kibinadamu pamoja na kushuhudia sadaka na majitoleo ya maisha yao.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Monsinyo Domenico Dal Molin, Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia wakati alipokuwa anatoa hotuba yake elekezi katika kongamano hili ambalo limewashirikisha watawa zaidi ya 800 kutoka sehemu mbali mbali za Italia. Wajumbe wamekumbushwa kwamba, hii ni dhamana pevu na endelevu inayohitaji kutekelezwa kwa ujasiri, uhodari, ugunduzi na ari ya kutaka kwenda mbali zaidi.

Kwa upande wake, Padre Josè Tolentino Mendonca amekemea kwa nguvu zote tabia ya watawa kutaka kujifungia katika ubinafsi wao. Hii inatokana na ukweli kwamba, watawa katika hija ya maisha na wito wao, wamejenga kuta katika mazingira yao, kiasi cha kujisikia kana kwamba, wanajitosheleza na wala hawahitaji msaada kutoka kwa watawa wengine. Matokeo yake ni watawa kuendelea kumezwa na upweke hasi na utendaji hafifu wa shughuli za kimissionari. Watawa wakumbuke kwamba, wito si kisiwa, kumbe, kuna haja ya kupambana na tabia ya kutaka kujitafuta binafsi, kwa kuimarisha mchakato wa maisha ya pamoja, kwani pasi na Jumuiya, watawa si mali kitu! Watapotea katika utupu na hali ya kukata tamaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.