2017-01-05 15:15:00

Unganisheni nyoyo na mikono katika ujenzi wa maeneo yenu!


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 5 Januari 2017 amekutana na kuzungumza na wananchi kutoka maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi hivi karibuni nchini Italia, amegusia mateso na mahangaiko ya watu; umuhimu wa kuwaheshimu na kuwasaidia katika mateso na mahangaiko yao; kuwafariji wale wanaolia na kuomboleza kwa kuondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao pamoja na kuonesha mshikamano wa upendo na wale wote waliopoteza kila kitu hata chembe ya matumaini!

Ili kuanza mchakato wa ujenzi wa maeneo yaliyoathirika kutokana na tetemeko la ardhi, kuna haja ya kuunganisha nyoyo na mikono! Ujenzi wa kwanza uanzie katika nyoyo za watu, ili kudumisha mafungamano ya kijamii na Kikanisa, mambo ambayo yametiliwa mkazo na mashuhuda mbali mbali waliopata nafasi ya kuzungumza mbele ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakumbuka madonda ya nyoyo aliyoyaona kwa watu wakati alipowatembelea kuwafariji kutokana na tetemeko la ardhi!

Hawa ni watu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki zao; walikuwa wamepoteza nyumba na vitega uchumi vyao. Hapa neno linaloongoza ni matumaini ili kuweza kuanza tena upya mchakato wa ujenzi unaofanywa kwa mikono ya binadamu! Ni ujenzi unaohitaji mshikamano wa umoja, udugu na upendo kama ilivyojionesha katika kazi ya uokoaji iliyofanywa na Kikosi cha uokoaji, jopo la madaktari na wauguzi bila kuwasahau watu wakujitolea. Ujenzi huu unahitaji mshikamano wa mikono na nyoyo za wananchi wote; mikono inayogusa na kuponya madonda kama alivyofanya Mwenyezi Mungu. Uponyaji huu unapaswa kufanywa kwa ushuhuda na matendo kwani maneno matupu yataendelea kusababisha makovu makubwa ya mahangaiko ya watu!

Kunahitajika ukimya, upole, upendo na unyenyekevu ili kuguswa na mahangaiko ya wengine anasema Baba Mtakatifu Francisko! Madonda yanaweza kupona, lakini kwa bahati mbaya, makovu yataendelea kuwepo, kama kumbu kumbu ya matukio haya magumu katika historia yao. Kuna haja ya kuwa na ujasiri, ari, uvumilivu, mshikamano pamoja na watu kusaidiana kwa hali na mali ili kuweza kukabiliana na changamoto ya ujenzi wa maeneo yaliyoathirika kwa tetemeko la ardhi nchini Italia.

Baba Mtakatifu anawasifu na kuwapongeza viongozi wa Kanisa waliosimama imara na kushikamana na wananchi walioathirika kwa tetemeko la ardhi, changamoto ni kuendelea kukuza na kudumisha ujirani mwema, ili kuwa kweli ni watu wema wenye ujasiri wa kuanza tena upya kama ndugu wamoja. Baba Mtakatifu anawataka wananchi hawa kuendelea kuwa na ndoto kwa kujiaminisha mbele ya Mungu katika shida na mahangaiko yao ya ndani, kama alivyofanya kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, baada ya kujisikia vibaya kutokana na madhara aliyoyaona kwenye eneo la tukio! Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote waliotoa shuhuda zao kwa niaba ya wenzao na kuwataka kusonga mbele kwa imani na matumaini katika ujenzi wa nyoyo za watu; ujenzi wa mafungamano ya kijamii; ujenzi wa maisha ya Kikanisa pamoja na kuondokana na ubinafsi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.