2017-01-05 17:09:00

Ni nyota iliyozua kizaa zaa kwa Herode!


Mtawala wa nchi anapotembelea na kutokea katika nchi nyingine hutanguzana na viongozi wengine wa juu, kama inavyosemwa: “Msafara wa mamba kenge hawakosekani.” Aidha mtawala huo afikapo aendako, hupokewa na mwenyeji wake kwa taadhima na hoihoi nyingi ikiwa ni pamoja na kupigiwa mizinga. Kwa lugha ya kigiriki kuonekana au kutokea huko kunaitwa Epifania.  Lakini Epifania ilimaanisha zaidi kule kuonekana kwa alama au vituko fulani vya ajabu kama vile mazingaombwe wakati wa vita au shida ya pekee iliyoikumba nchi au taifa. Kwa hiyo, katika ulimwengu wa kipagani Epifani ni kuonekana kwa vioja au miujiza iliyosababishwa na miungu.

Leo tunaadhimisha sikukuu ya Epifania yaani Tokeo la Bwana. Lakini Epifania hii ya Kristo ni ya kawaida kabisa haina miujiza wala vioja vyovyote vile. Msafara wa Yesu wa kuja duniani ni wa kawaida kabisa. Yesu alizaliwa kama watoto wengine wanaozaliwa katika familia ya kimaskini. Kisha akaviringishwa vitambaa na kulazwa kwenye hori la kulishia wanyama. Huu ndiyo ufunuo na kujitambulisha duniani kwa mwanga wa upendo wa Mungu usio na mipaka.  

Fasuli ya Injili ya leo, inataka kutuonesha namna ya kuupokea upendo huo wa Mungu uliotutokea duniani. Namna mojawapo ya mapokezi inawakilishwa na kundi la watu wanaoitwa Majusi. Kundi hili lilikuwa na Majusi watatu, Melkior, Baltazar na Gaspar. Melkior anaoneshwa kuwa mzee wa umri mwenye ndevu nyeupe. Mamajusi huyu anatoa zawadi ya dhahabu. Kisha Baltazar ni mtu mzima mwenye umri wa kati anayo ngozi ya rangi nyeusi, naye anamzawadia Yesu manukato. Majusi wa tatu ni Kaspar anaoneshwa kuwa ni kijana anamtolea Yesu zawadi ya ubani. Tofauti yao ya umri na utaifa, inawakilisha aina tatu tofauti za mataifa ya watu wanaomwendea Yesu. Aidha kutokana na umri wao tofauti huonesha kuwa watu wote awe mzee, mtu mzima au kijana hutafuta mwanga yaani hutafuta nyota ya maisha yao. Kwa hiyo sisi sote tunahitaji kufuata nyota ya maisha yetu.

 Mamajusi hawa walipofika Yerusalemu, nyota iliyowaongoza iliwapotea, ndipo walipoanza kuuliza: “Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mamajusi hawa waliiona nyota mashariki, maana yake taiba yao ilikuwa ni kuangalia angani. Huko kuangalia angani kunaonesha kwamba walikuwa wanamtafakari uumbaji hadi wakaugundua mwanga wa Mungu mwumbaji na kuutangaza. Kwa hiyo anayetaka kulingana na mamajusi yambidi adhamirie zaidi mambo ya uumbaji wa Mungu yaani maana ya maisha yake. Pili, mamajusi walikuwa wanasukumwa na mambo ya Mungu yanayowapa maana ya maisha yao na wakayachukulia hatua. Tatu, hawakutulia pahala pamoja bali daima walisafiri kutafuta ufalme mpya na mwanga mpya. Baada ya kujua kwamba amezaliwa mfalme wanataka kumfahamu zaidi yaani  wanafanya utafiti.

Kundi jingine ni la wakuu wa serikali au wa siasa na wa dini, yaani Herode, wakuu wa makuhani, waandishi na watu wote wa Yerusalem. Mamajusi waliiona nyota angani, “tuliiona nyota yake mashariki.” lakini wasomi yaani wakuu wa makuhani na waandishi waliitafuta nyota hiyo katika maandishi. Mathalani katika biblia kitabu cha Hesabu. Kituko cha Balam na Barak wa Moab huzungumza juu ya nyota itakayotakiwa itokee huko Israeli. Ingawaje mtunzi wa sehemu hiyo alifikiria nyota hiyo ingekuwa ni Yosia, kumbe haikutimilika. Hivi Waisraeli wakaendelea kusubiri tu kutokea kwa nyota hiyo. Sasa nyota hiyo imetokea kwa majusi nao wanataka kumpokea masiha na kumwabudu. Mamajusi wanashangazwa na nyota mpya inayotoa mwanga unaoangaza ulimwenguni mzima. Hii ndiyo Epifania ya Mungu yaani ni ufunuo ambao ni upendo aliouleta Yesu.

“Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.” Mkuu huyu anawawakilisha watu wote walio katika ngazi mbalimbali za utawala wa serikali, wa siasa waliolewa vyeo, na watu wa dini wasiotaka mabadiliko na wanamhusisha Mungu ili kutetea maslahi yao. Kutokana na kufadhaika huko, Herode “Akakusanya Wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo amezaliwa wapi?” Wakuu na wataalamu hao wanafahamu maandiko matakatifu, lakini wanapoteza bahati ya kufungua mioyo yao na kupokea mwanga wa Mungu. Kisha Herode akawaita Majusi faraghani na kuwaagiza kuwa watakapomwona mtoto wamrudie kumpa habari zake ili naye aende kumwabudu. Hapa unaona jinsi watawala wanavyobomoa uwongo ili kutetea maslahi yao. Huu ndiyo ufalme wa kale, ulio katika giza, unaofanya mambo yake gizani na siyo mwangani.

Yerusalemu inawakilisha mahali penye taasisi za dini na serikali ambapo mwanga wa nyota ya Kristu hauwezi kung’aa. Ndiyo maana majusi wanapoingia Yerusalemu mjini nyota haiwaki tena hadi wanapotoka tena nje ya mji. Nyota hiyo inawaongoza hadi pahala alipolazwa mtoto. Kwa furaha kubwa wanapiga magoti kumwabudu na kumtolea zawadi. Kuna tafsiri tofauti juu ya zawadi zilizotolewa. Lakini tafsiri ya kibiblia ni hii kwamba, taifa la Wayahudi linajulikana kuwa ni la kifalme, la kikuhani na ni bi arusi wa Mungu. Dhahabu inawakilisha mfalme, ubani ni alama ya kuhani na bi-arusi wa Bwana ni kama harufu nzuri ya manukato. Kwa hiyo zawadi hizi tatu zinawawakilisha wapagani wale wote wanaopokea mwanga wa nyota hii, wanakuwa taifa jipya la kifalme, la kikuhani na bi arusi wa Bwana. Wakristu katika Agano jipya ni taifa la ufalme mpya, ukuhani wa taifa jipya, na bi-arusi mpya wa mwanakondoo. Heri kwa sikukuu ya Epifania.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.