2017-01-04 14:13:00

Mshikamano na faraja kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Italia


Mama Kanisa tarehe 6 Januari 2017 anaadhimisha Siku kuu ya Tokeo la Bwana, maarufu kama “Epifania”, Siku ya Mwanga, Mwana wa Mungu alipojifunua kwa Mataifa na Mamajusi wakamletea zawadi muhimu sana zinazodhihirisha maisha na utume wake hapa duniani! Mamajusi walimtolea Ubani, alama ya Umungu wa Kristo kwani Yesu Kristo ni Nafasi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; Mwana kondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu, sadaka safi inayompendeza Baba wa milele!

Mamajusi walimtolea Mtoto Yesu zawadi ya dhahabu: kielelezo cha Ufalme wa Kristo ambao ni wa milele na wa ulimwengu wote. Huu ni Ufalme wa kweli na uzima; ufalme unaosimikwa katika utakatifu na neema ya Mungu. Ni Ufalme unaofumbatwa katika misingi ya haki, upendo na amani. Zawadi ya tatu aliyopewa Mtoto Yesu ni Manemane, kielelezo cha ubinadamu wa Yesu Kristo aliyezaliwa kwa Bikira Maria, katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Ni ubinadamu unaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko, kielelezo cha matumaini mapya na kiini cha imani na maisha ya Kikristo!

Ni katika mazingira ya mkesha wa Siku kuu ya Tokeo la Bwana, Baba Mtakatifu Francisko anakutana na familia ya Mungu kutoka katika maeneo yaliyoathirika kwa tetetemeko la ardhi hivi karibuni nchini Italia. Askofu mkuu Renato Boccardo wa Jimbo Katoliki Spoleto-Norcia anasema, huu ni mkutano wa upendo na mshikamano kwa wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki zao; waliopoteza makazi na usalama wa kiuchumi kwani vitega uchumi vyao, vimefunikwa na kifusi cha udongo. Hawa ni watu wanaoishi katika makazi ya muda, wakiteseka kwa changamoto mbali mbali.

Ni wananchi ambao wamepata majeraha baada ya kuangukiwa na vifusi vya majengo; wote hawa wanasubiri neno la faraja na matumaini kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Zaidi ya watu 800 walioathirika kwa tetemeko la ardhi nchini Italia wakiongozwa na Askofu mkuu Renato Boccardo wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Siku kuu ya Tokeo la Bwana. Huu ni mkutano wa upendo utakaowashirikisha wadau mbali mbali ambao wamekuwa mstari wa mbele kupandikiza mbegu ya huduma, faraja na upendo kwa waathirika wa tetemeko la ardhi. Lengo la Kanisa ni kuendelea kuwatia shime wadau mbali mbali ili kujizatiti zaidi: kiroho na kimwili katika kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi. Tukio hili la huruma na upendo, litahitimishwa Jumapili tarehe 8 Januari 2017, Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia, Italia akisaidiana na Askofu mkuu Renato Boccardo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.