2017-01-04 13:57:00

Changamoto ya magereza nchini Brazil!


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil limesikitishwa sana na mauaji ya kinyama yaliyotokea kwenye Gerezani Manaus na kusababisha zaidi ya wafungwa 56 kupoteza maisha yao kwa kuuwawa kikatili. Akizungumzia juu ya tukio hili, Askofu msaidizi Jose Albuquerque AraĆ¹jo wa Jimbo Katoliki la Manaus anasema, familia ya Mungu Jimboni humo inaungana na wote walioguswa na kutikishwa na mkasa huu wa kusikitisha sana kutokana na mauaji ya kikatili yaliyofanywa na makundi mawili ya kiuhalifu yaliyopambana gerezani humo.

Kuna changamoto kubwa zinazopaswa kufanyiwa kazi na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na usalama, amani na utulivu kwenye magereza nchini Brazil. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, Serikali kuu itaweza kuivalia njuga changamoto hii na kuipatia suluhu ya kudumu, ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia kuendelea kupotea wakiwa gerezani. Kuna wafungwa pamoja na familia zao wanaathirika vibaya kutokana na kinzani zinazoendelea chini kwa chini huko gerezani, kiasi cha kusababisha hofu na wasi wasi mkubwa!

Kanisa nchini Brazil, linapenda kutoa mwaliko kwa familia ya Mungu nchini humo kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano, kwa kujikita katika kanuni maadili na haki msingi za binadamu. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, magereza yanakuwa ni mahali pa utulivu na haki kwa kuzingatia na kuheshimu zawadi ya maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa wafungwa hata wanapokuwa gerezani! Serikali kuu ikiweza kuivalia njuga changamoto hii, magereza nchini Brazil, yanaweza kuwa kweli ni taasisi ya mafunzo, nidhamu na mafungamano ya kijamii kwa wafungwa wanaomaliza adhabu zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.