2017-01-02 09:06:00

Ni kwa ajili ya huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu!


Familia ya Mungu nchini Argentina, imeuanza Mwaka 2017 kwa kupata gazeti la L’Osservatore Romano linalomilikiwa na Vatican, gazeti ambalo litakuwa linatolewa kila juma, ili kuwawezesha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupata habari ya maisha na utume wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, kufahamu shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa toleo la kwanza la Gazeti hili huko nchini Argentina, anapenda kutoa salam na baraka kwa wadau mbali mbali waliojisadaka ili kuhakikisha kwamba, gazeti la L’Osservatore Romano linaifikia familia ya Mungu nchini Argentina. Hii ni huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani.

Baba Mtakatifu anawaweka wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu. Anawaomba wamkumbuke katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sala na sadaka yao! Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, limepokea kwa mikono miwili toleo hili la Gazeti la L’Osservatore Romano litakalokuwa linahaririwa na Marcelo Figueroa, mtaalam wa Biblia, lakini si Mkatoliki. Hii ni changamoto ya ujenzi wa Uekumene wa huduma na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu.

Anasema, jambo la msingi ni kuwa waaminifu katika utekelezaji wa dhamana na wajibu huu wa kuchapisha nyaraka za Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa uaminifu mkubwa pamoja na kuzama zaidi katika tasaufi ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Kwa mara ya kwanza Gazeti la L’Osservatore Romano tangu kuanzishwa kwake miaka  155 iliyopita litachapisha habari pia za watu mahalia nje ya habari za Vatican. Utakuwa ni uwanja wa kukuza na kudumisha pia mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini na watu wote wenye mapenzi mema, kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Baba Mtakatifu katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo, umoja, udugu na mshikamano kati ya watu.

Kwa upande wake, Victor Manuel Fernàndèz, Mkuu wa Chuo kikuu cha Kikatoliki Argentina anasema, toleo la Gazeti la L’Osservatore Romano nchini Argentina, litasaidia kukoleza na kuimarisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana; msamaha na mshikamano; kwa kufahamiana ili kujadiliana; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuwa kweli ni sauti ya wanyonge.

Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kudumisha utamaduni wa kazi na makazi ambao ni utimilifu wa maisha ya binadamu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote dhamana inayovaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko, bila kusahau utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kujisomea na kutafakari kile ambacho Baba Mtakatifu anaandika na kufundisha. Ni kiongozi anayelitaka Kanisa kujitegemea kwa kuwa na rasilimali fedha na watu kwa njia ya halali na kamwe isiwe ni fedha inayonuka rushwa na ufisadi. Ni afadhali kuwa na Kanisa maskini kwa ajili pamoja na maskini, kuliko Kanisa tajiri linalonuka damu ya mafisadi!

Gazeti la L’Osservatore Romano linajitahidi kutoa picha halisi ya mawazo na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Ni kiongozi mwenye imani, matumaini na mapendo; asiyependa makuu; ni mtu wa watu kwa ajili ya watu, ili aweze kuwapeleka wote kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu! Ni kiongozo anayeendelea kuhamasisha ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa haki, amani na mshikamano kwa njia ya ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Huu ni mradi ambao kwa miaka mingi ulikuwa unafanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kuanzia mwaka 1931 na kuanza kuchapishwa kwa mara ya kwanza kunako tarehe 4 Novemba 1951. Baadaye likafanyiwa marekebisho na maboresho makubwa kunako mwaka 1969 likaanza pia kuchapishwa kwa ajili ya nchi za Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.