2017-01-02 11:54:00

Jubilei ya miaka 200 ya Shirika la Mabruda wa Maria!


Shirika la Mabruda wa Maria “Marist Brothers” linaadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwake kunako tarehe 2 Januari 1817 huko nchini Ufaransa na Mtakatifu Marcellin Champagnat akiwa na lengo na kuelimisha na kuinjilisha vijana wa kizazi kipya, hasa wale waliokuwa na mahitaji Zaidi. Kunako mwaka 1863 Shirika lilipewa hadhi na kutambuliwa kuwa ni Shirika la Kipapa. Hadi sasa kuna jumla ya wanashirika 3, 080 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi 81 duniani. Hili ni Shirika linaloshirikiana kwa karibu sana na waamini walei katika mchakato wa elimu na uinjilishaji.

Br. Emili Turù, Mkuu wa Shirika la Mabruda wa Maria katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho haya anasema, wanayo maneno makuu matatu: shukrani, msamaha na majitoleo yanayoonesha dira na mwelekeo wao katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika lao. Wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Mtakatifu Marcellin, Muasisi wa Shirika lao aliyesaidia mchakato wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, ili aweze kufahamika kati ya mataifa na kupendwa na wengi, hasa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Shirika linamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye katika kipindi cha Miaka 200, Watawa 38, 000 wameweka nadhiri zao za daima kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani! Wanapenda kujizatiti katika kuwalinda na kuwahudumia watoto na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya elimu na Uinjilishaji. Maadhimisho haya yanaanza rasmi tarehe 2 Januari 2017 na kuendelea sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.