2017-01-01 09:50:00

Waamini mnaye Mama B. Maria ondoeni Saratani ya maisha ya kiroho!


Bikira Maria ni Mama aliyejitahidi kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake na akafaulu kuyamwilisha siku kwa siku, ili kuweza kuwa ni daraja la Mungu katika maisha ya watu wake. Alijifunza kusikiliza mapigo ya Mwanaye mpendwa alipokuwa angali mchanga tumboni mwake, na hiki kikawa ni kigezo muhimu katika kufahamu mapigo ya Mungu katika historia. Akajifunza kuwa ni Mama na Mtoto Yesu akamkirimia zawadi ya kumtambua kuwa ni Mama yake mpendwa. Kwa njia ya Bikira Maria, Neno wa Mungu alifanyika mwili, akajifunza pia kutambua upendo wa kimama kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtoto Yesu pamoja na Bikira Maria alijifunza kusikiliza kwa makini mapigo, mahangaiko, furaha na matumaini ya Taifa teule la Mungu. Kwa njia ya Bikira Maria, Yesu akajitambua kuwa ni Mtoto wa Taifa aminifu la Mungu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa takatifu ya kuadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos”, tarehe Mosi, Januari 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, sanjari na maadhimisho ya Siku ya 50 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2017. Bikira Maria kadiri ya Maandiko Matakatifu anaonekana kuwa ni mwanamke asiyependa makuu, mtu wa maneno machache wala si mhusika mkuu katika matukio mbali mbali, lakini alikuwa ni na jicho makini lililotambua kutunza maisha na utume  wa Mwanaye na kile ambacho Yesu alipenda!

Bikira Maria alitunza matumaini ya Jumuiya ya kwanza ya Wakristo na hivyo akajifunza kuwa kweli ni Mama wa wengi! Alikuwa karibu na matukio mbali mbali ili kupandikiza mbegu ya matumaini. Akadiri kusindikiza Misalaba iliyoibuliwa kutoka katika nyoyo za watoto wake katika hali ya ukimya, Bikira Maria akawa ni chemchemi ya Ibada inayojionesha katika Madhabahu na Makanisa sehemu mbali mbali za dunia; mambo yanayodhihirisha ukweli huu.

Bikira Maria amewakirimia waamini joto la kimama linalomzunguka mwamini wakati wa shida na magumu; joto ambalo ni ngao inayolinda mchakato wa mageuzi ya upendo kwa Mwanaye mpendwa, kwani mahali palipo na Mama hapo kweli kuna upendo. Bikira Maria kwa njia ya umama wake anaonesha kwamba, unyenyekevu na upole si fadhila ya wanyonge, bali ya watu wenye nguvu lakini anaonya kwamba, si haki kuwatendea wengine ubaya ili kujisikia kuwa ni mtu muhimu sana! Watu wa Mungu daima wamemtambua Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kwa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu na binadamu, mwanzoni mwa Mwaka, maana yake ni kukumbuka uhakika wa kuwa na Mama atakayewasindikiza katika safari yao, kwani wao ni watu wenye Mama  na kamwe si watoto yatima! Umama wa Bikira Maria ni kinyume kabisa cha ubinafsi, hali ya kujifunga na kujitafuta mwenyewe. Jamii isiyokuwa na mama ni pweke, imepoteza “moyo na ladha ya familia” haina ibada, kwani akina Mama katika hali ngumu ya maisha wanao uwezo wa kushuhudia upendo na majitoleo pasi na masharti kwani ni nguvu ya matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, amejifunza kwa kiasi kikubwa kutoka kwa akina mama ambao walikuwa na watoto wao wamefungwa gerezani, wakiwa wamelazwa hospitalini au wametumbukizwa katika dimbwi la utumwa wa matumizi haramu ya dawa za kulevya; watoto wanaokabiliwa na joto, baridi kali na ukame; katika matukio yote haya, akina mama hawa walijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya watoto wao. Hawa ni sawa ni akina mama kwenye kambi za wakimbizi au waliko katikati ya vita, daima wako pamoja na watoto wao katika shida na mahangaiko haya, tayari kusimama kidete ili asiwepo na mtoto anayepoteza maisha; kwani wao ni chombo cha umoja na mali ya watoto wao.

Kuuanza Mwaka Mpya kwa maadhimisho ya wema wa Mungu katika sura ya Bikira Maria, kunakojionesha pia katika sura ya Kanisa pamoja na akina mama wengine, kunawalinda waamini dhidi ya ugonjwa wa “Uyatima wa maisha ya kiroho” pale waamini wanapojisikia kutokuwa na mama na hivyo kushindwa kuonja upendo wa Mungu. Huu ni ugonjwa unaowakumba wale ambao wanashindwa kuwa na utambulisho wa familia, jamii ya watu, mahali na kwa Mungu wao. Huu ni ugonjwa unaojikita katika moyo wenye ubinafsi unaojiangalia na kutafuta mafao yake binafsi na kwamba, ugonjwa huu unaweza kukua na kuongezeka, pale watu wanaposahau kwamba, maisha ni zawadi ambayo wameipokea kwa ajili ya wengine na kwamba, wanapaswa kuishirikisha katika nyumba ya wote!

Uyatima wa maisha ya kiroho ndio uliopelekea Kaini katika Agano la Kale kutotambua wajibu wake mbele ya ndugu yake Abeli. Hii saratani inayoharibu moyo wa binadamu na matokeo yake ni uharibifu pia wa mazingira nyumba ya wote; uharibifu wa utu na heshima ya binadamu kwa vile tu si ndugu wala jamaa na hatimaye, ugonjwa huu unawaharibu hata wao wenyewe kutokana na upweke hasi, kwani kunakosekana mwingiliano wa dhati kiasi cha kupoteza upendo, ladha, ibada na huruma. Uyatima wa maisha ya kiroho anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko unawafanya watu kupoteza kumbu kumbu ya maana na utambulisho wao kama jamii na waamini; umuhimu wa michezo, furaha, mapumziko na majitoleo.

Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu yanawawezesha waamini kuibuka tena wakiwa na nyuso za furaha kwa kujitambua kuwa ni watu, sehemu ya Jumuiya na familia ili kupata fursa ya kujifunza kukua na kujisadaka kwa ajili ya wengine; kuna wakumbusha kwamba, wao ni watoto, ni familia na watu wa Mungu na wala si bidhaa au wadadisi wa habari! Hii ni fursa ya kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii yanayotoa utambulisho wa watu; makazi katika miji pamoja na kujisikia kuwa ni Jumuiya inayowaunganisha na kuwaenzi.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa mahubiri yake anasema, Yesu Kristo alipokuwa pale Msalabani kabla ya kuyamimina maisha yake, alimkabidhi Bikira Maria kwa wafuasi wake, mwaliko wa kumpokea na kumkaribisha Bikira Maria katika familia, jumuiya na katika nchi mbali mbali, ili kukutana na uso wake wa Kimama unaowaokoa kutoka katika ugonjwa wa uyatima wa maisha ya kiroho, unaowakumbusha kwamba wao ni ndugu wamoja. Ni uso unaowafundisha kujifunza kuhudumiana kwa upendo katika maisha kama Bikira Maria alivyofanya: kwa kupandikiza matumaini, utambulisho na udugu! Waamini watambue kwamba, wanaye Bikira Maria, Mama wa Mungu kama walivyokiri waamini wa Efeso!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.