2017-01-01 10:05:00

2017: Waamini wanamlilia Mungu awajalie: Imani, Haki, Amani na Udugu!


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, tarehe Mosi Januari 2017, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, waamini wamesali kwa ajili ya kuliombea Kanisa ili liweze kuzaa watoto wapya, wanaolindwa na Mungu katika utimilifu wa imani, furaha na mapendo ya kishujaa. Wamewaombea watunga sheria, viongozi wa serikali na mahakimu, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaonesha ukweli, kuwaongezea kiu ya haki na kuwaimarisha katika ari ya huduma.

Tarehe Mosi Januari, 2017 ni Siku ya 50 ya Kuombea Amani Duniani, waamini wamesali kwa ajili ya kumlilia Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki na amani, ili aweze kufutilia mbali mnyororo wa vita, kwa kuokoa akili na nyoyo za watu kutokana katika giza la chuki na uhasama, kwa kuwapatia njia na mwelekeo mpya unaofumbatwa katika udugu na upatanisho. Imekuwa ni siku pia ya kuombea miito mbali mbali ndani ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, wito wa Upadre na Utawa, ili kweli Mwenyezi Mungu apeleke watenda kazi katika shamba lake, kwa kuwawezesha vijana kufanya maamuzi magumu katika maisha mintarafu mwanga wa Injili ili kutambua furaha ya kujisadaka na kupenda pasi na masharti!

Mwishoni, kwa lugha ya Kiswahili, Sr. Marxilliana Massawe kutoka Tanzania amesali kwa ajili ya kumwomba Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwabariki wanawake ambao ni chemchemi ya uhai, awajalie fadhila ya upendo katika kuwatunza watoto na uthabiti wa ukomavu katika malezi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.