2016-12-31 14:45:00

UN yampongeza Rais mteule Adama Barrow wa Gambia!


Umoja wa Mataifa utaendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na amani na utulivu wakati wa kuachiana madaraka nchini Gambia, kwa wakati na muda uliopangwa. Bwana Adama Barrow aliyeshinda uchaguzi mkuu nchini Gambia ni kiongozi halali anayepeswa kuchukua madaraka ya nchi kwa mujibu wa Katiba ya Gambia! Katibu mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amempongeza kwa Barrow kwa kuibuka kidedea wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Gambia uliohitimishwa hivi karibuni na matokeo kutangazwa.

Umoja wa Mataifa unamtaka Rais mteule Barrow kuwadhibiti wafuasi wake, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu nchini Gambia, ili isije ikajikuta inatumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo ni hatari kubwa sana! Msimamo wa Umoja wa Mataifa unaungwa mkono na msimamo wa Jumuiya ya Uchumi Afrika magharibi, ECOWAS iliyokutanika hivi karibuni nchini Nigeria na kutoa msimamo wake kwamba, Rais mteule Barrow alikuwa ameshinda uchaguzi mkuu na kwamba, taratibu, kanuni na sheria zote zitatekelezwa ili kuhakikisha kwamba, anaingia madarakani kwa amani na utulivu, hapo tarehe 19 Januari 2019.

Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Rais mteule ni kuhakikisha kwamba, anajenga na kudumisha utawala wa sheria, demokrasia, haki, amani na maendeleo endelevu nchini Gambia. Kwa muda wa miaka 22 Rais Yahya Jammeh ameiongoza Gambia na hatimaye, kupigwa mweleka chali na Bwana Barrow katika uchaguzi uliohitimishwa hivi karibuni. Mwanzo alikubali matokeo ya uchaguzi mkuu lakini baadaye akabadili uamuzi wake na kususia matokeo. ECOWAS imesema itatuma vikosi vya kijeshi ili kuhakikisha kwamba,  amani, utulivu na haki vinataala wakati wa kukabidhiana madaraka nchini Gambia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.