2016-12-31 14:09:00

Miaka 10 ya Utawala wa Ban Ki-Moon Umoja wa Mataifa!


Bwana Ban Ki-Moon baada ya kuhudumia kama Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa muda wa miaka 10, Januari Mosi, 2017 anang’atuka rasmi madarakani na Professa Antonio Guterres anaingia madarakani kwa muda wa miaka mitano! Bwana Ban Ki-Moon anasema, katika kipindi cha uongozi wake kwa miaka kumi, kumekuwepo na mafanikio makubwa, lakini jambo ambalo linamsikitisha hadi anang’atuka kutoka madarakani ni vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inayoendelea kujionesha sehemu mbali mbali za dunia.

Vita huko Siria, Sudan ya Kusini, Yemen, DRC, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na huko Mashari ya Kati ni changamoto ambayo hakupatia ufumbuzi wa kudumu katika uongozi wa Bwana Ban Ki-Moon. Haya ni matokeo ya baadhi ya viongozi wakuu wa nchi kupenda mno utajiri na madaraka na kusahau kuwahudumia wananchi wao, kutafuta mafao na ustawi wengi.

Ushirikiano na mshikamano wa kimataifa ni nyenzo msingi katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano katika Jumuiya ya Kimataifa; mambo msingi katika harakati za maendeleo endelevu! Dunia inahitaji viongozi wanaojikita katika utawala wa sheria, demokrasia na katiba za Nchi yao; viongozi wazalendo na wenye uchu wa nchi zao! Kuna viongozi ambao duniani wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa kama vile Abraham Lincoln, shujaa aliyeonesha umuhimu wa kujenga na kudumisha usawa, mafungamano ya kijamii na maridhiano! Hizi ni tunu ambazo zinahitajika hata katika ulimwengu mamboleo.

Bwana Ban Ki-Moon alitoa kipaumbele cha pekee katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi; kwa kusimama kidete kutetea usawa wa kijinsia na fursa sawa kati ya wanawake na wanawaume; pamoja na kudumisha utawala wa sheria. Itifaki ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Paris, Ufaransa kwa mwaka 2015; Malengo ya Maendeleo Endelevu: Kupambana na umaskini, kulinda na kutunza mazingira na utawala bora ni mambo ambayo amefanikiwa kuyapatia mwelekeo wa pekee katika Jumuiya ya Kimataifa, sasa inatakiwa utekelezaji wake!

Wachunguzi wa mambo wanamshutumu pia Bwana Ban Ki-Moon kwa kushindwa kukemea uvunjifu wa haki msingi za binadamu nchini Russia; kwa kushindwa kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Kipindu pindu nchini Haiti na hivyo kusababisha watu wengi kupoteza maisha yao! Baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walishutumiwa kwa kufanya nyanyaso za kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana sehemu mbali mbali za dunia, Falme za Kiarabu kujihusisha na mauaji ya watoto wasiokuwa na hatia huko Yemen.

Ban Ki-Moon alisafiri sana duniani kwa kuamini kwamba, mazungumzo ya moja kwa moja yalikuwa na mafanikio makubwa zaidi. Baadhi ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wanasema, Ban Ki-Moon hakuwa na uwezo mkubwa wa mawasiliano na watu na wala hakuwa kiongozi mwenye karama mambo msingi kwa watu wa nyakati hizi. Pamoja na mapungufu yote haya, lakini viongozi wengi wanasema ni kiongozi aliyejisadaka katika kuhudumia Umoja wa Mataifa, kwa kutafuta mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Silaha yake kubwa ilikuwa ni kuheshimu wengine kama kielelezo makini cha uongozi. Mchakato wa upatanisho kati ya Korea ya Kusini na Kaskazini umekwama mchangani! Je, Ban Ki-Moon anaporejea nchini mwake, anaweza kuchaguliwa kuwa Rais wa Korea ya Kusini, ili kuzima mzuka wa wananchi ambao wamekuwa wakindamana usiku na mchana kupinga utawala wa Rais aliyeko madarakani?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.