2016-12-31 08:19:00

Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia Amani Duniani!


Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1967 alianzisha kwa mara ya kwanza Siku ya Kuombea Amani Duniani sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, ili familia ya Mungu inapoanza Mwaka Mpya iweze kupata neema na baraka ya kutembea katika misingi ya haki, amani na upatanisho kama kikolezo na chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu, kwa kutambua kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo! Kwa bahati mbaya amani inakabiliwa na upinzani na changamoto nyingi duniani, ndiyo maana Kanisa kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema linataka kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili kweli awajalie binadamu amani ya kweli inayobubujika kutoka kwake.

Kanisa Katoliki shuhuda na chombo cha amani, linataka kuanzisha mchakato wa dhana ya amani duniani inayopaswa kupokelewa kwa mikono miwili na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe Mosi Januari, familia ya Mungu duniani isali kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, vita vina hatari na madhara makubwa katika maisha ya watu. Maadhimisho ya Siku ya kuombea amani ni sehemu ya utambulisho wa imani na maadili ya Kikristo anasema Mwenyeheri Paulo VI katika ujumbe wake wa Kuombea Amani Duniani uliochapishwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1967.

Hapa waamini pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, wanapaswa kusimama kidete kulinda na kudumisha amani duniani kwa kuondokana na ubinafsi unaogumisha mahusiano mema ya kidplomasia kati ya mataifa. Ni wajibu wa kusimama kidete kulinda Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu dhidi ya vita na kinzani za kijamii inayoweza kusababishwa na nguvu za kivita, kiuchumi na kisiasa kiasi hata cha kutozingatia mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Kinzani na migogoro ya kitaifa na kimataifa itatuliwe kwa njia ya majadiliano katika ukweli na haki kwa kuzingatia utawala wa sheria na usawa kwani kimsingi amani inafumbatwa katika maisha kwa kutambua na kutekeleza kwa dhati haki na wajibu.

Kuna haja ya kuwafunda vijana wa kizazi kipya utamaduni wa amani, heshima, umoja, udugu, ushirikiano na mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Siku ya Kuombea Amani Duniani inalenga kuenzi vyombo vya ulinzi na usalama; taasisi za kitaifa na kimataifa katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake yanayopania kujenga amani duniani, kwani amani inajengwa kwa njia ya matendo na wala si kwa maneno matupu ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa!

Amani ya kweli inafumbatwa katika ukweli, upendo na haki kati ya Jumuiya ya Kimataifa na watu wake, ili kukuza na kudumisha uhuru wa watu wake katika masuala ya kiraia, kitamaduni, kimaadili na kidini. Hapa kuna umuhimu wa kudumisha utu na heshima ya binadamu pamoja na utawala wa sheria ili kuondokana na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Lengo ni kukuza na kudumisha amani ya kweli, katika haki, usawa pamoja na kutambua haki msingi za binadamu. Wananchi wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya kulinda na kudumisha haki na uhuru unaowajibisha mintarafu ukweli na upendo.

Mwenyeheri Paulo VI anakaza kusema, Siku ya Kuombea Amani Duniani inakwenda sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, muda muafaka wa kuombea amani duniani. Hii ni dhamana anayoitekeleza kwa kutambua utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anayeguswa na mahangaiko ya watu wanaoteseka kutokana na vita, kinzani na mipasuko wa kijamii; watu ambao utu na heshima yao kama watoto wapendwa wa Mungu “unatiwa mchanga”. Anataka kweli familia ya Mungu ijikite katika ujenzi wa amani, umoja na mshikamano kati ya watu badala ya ubinafsi unaojikita katika vita na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko.

Kanisa linapenda kutangaza na kushuhudia amani kwani hii ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu na Kristo ni amani ya watu wake na Injili yote inafumbatwa katika fadhila ya amani ambayo imefikia kilele chake pale Mlimani Kalvari, juu la Msalaba alipoupatanisha ulimwengu na Baba yake wa mbinguni kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Kristo kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani duniani, ili kuondokana na utamaduni wa kifo. Watu wajenge utamaduni wa: kupenda kuzungumzia, kuelimisha na kumwilisha tunu ya amani katika maisha kama alivyokazia Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume, “Amani Duniani”, “Pacem in terris”.

Kanisa Katoliki kwa mara ya kwanza lilianza kuadhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani kunako mwa 1968, ili kukuza umoja, udugu na mshikamano; kwa kutambua upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu wote. Umoja huu unafumbatwa katika nia na matendo; ili kukuza upendo kwa Mungu na jirani; msamaha na upatanisho; mambo msingi yanayopyaisha tunu msingi za maisha ya kijamii. Sala ya kuombea amani duniani ina nguvu ya kimaadili. Itakumbukwa kwamba, mwaka 1968 ulikuwa ni Mwaka wa Neema chemchemi ya matumaini na hivyo ikawa ni fursa makini kwa ajili ya kuombea amani duniani. Kila mtu asema “Dona nobis pacem”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.