2016-12-31 11:07:00

Huduma na utume wa Mapadre!


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri anasema, dhamana, maisha na utume wa Wakleri ni kutembea pamoja na familia ya Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wadhaifu na wagonjwa ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii yanayojikita katika kipaji cha ugunduzi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji! Wakleri wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha ari na moyo wa umoja, upendo na udugu kati ya watu wa Mungu wanaowaongoza.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kweli Wakleri wanakuwa na ari na moyo wa kimissionari na kichungaji, unaowasukuma na kuwabidisha zaidi na zaidi kuwaendea wale walioko pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha, kama anavyowahimiza Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Stella ameyasema haya hivi karibuni alipokutana na kuzungumza na Wakleri wa Jimbo kuu la Napoli, lililoko Kusini mwa Italia.

Kardinali Stella amewakumbusha kwamba, kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko ni mfano wa kuigwa katika maisha na utume wa Kipadre, kwani anawachangamotisha kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo msingi katika wito na utume wa Kipadre, yaani moyo wa sadaka na huduma kwa familia ya Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kuna mamilioni ya watu wenye kiu ya kutaka kusikiliza Neno la Mungu linalotangazwa na kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha yenye mvuto na mashiko!

Watu wengi wamekata na kujikatia tamaa; wanateseka na kuhangaika kutokana na sababu mbali mbali; ni watu wanaofanana “kama daladala iliyokatika usukani” na hivyo hawana dira na mwelekeo sahihi wa maisha. Hawa ni watu wanaotaka kuona Kanisa lililopyaishwa katika maisha na utume wake, Kanisa linalowajali na kuwahudumia maskini kwa ajili pamoja na maskini, kwani hata maskini katika umaskini wao wanalo jambo wanaloweza kuchangia.

Kanisa anasema Baba Mtakatifu linapaswa kuwa ni hospitali ya matumaini kwa wale walioko kwenye Uwanja wa vita, tayari kuwaganga na kuwaponya wanaosumbuka kiroho na kimwili. Hii ni changamoto ya kugundua na kupyaisha maisha, utume na utambulisho wa wakleri, ili kutekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo makini cha Mchungaji mwema, anayejisadaka kwa ajili ya Kondoo wake.

Mambo makuu yanayopewa kipaumbele cha pekee katika maisha  na utume wa Kipadre ni: Upendo kwa Kristo na Kanisa lake; huruma na upendo; sadaka, ari na moyo wa kimissionari, tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wkkovu bila ya kujibakiza! Mambo haya yatawasaidia Wakleri kutekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya Kristo na Kanisa lake; kwa kuwa ni Wasamaria wema wanaothubutu kujitaabisha kuwatafuta, kuwaganga na kuwaponyesha wale wote wanaoteseka katika mapambano ya maisha. Wakleri wawe na ujasiri wa kimissionari, tayari kujikita katika mambo msingi ya maisha na utume wa Kipadre.

Wawe tayari kuvutwa na Mwenyezi Mungu pamoja na binadamu anayening’inia kwenye ombwe la maisha; kati ya Mungu  na malimwengu. Mapadre wawapende na kuwahudumia watu wao kwa kujikita katika tasaufi ya maisha ya Kipadre na kuzingatia sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Huu ni mchakato unaopania kuboresha maisha ya kiroho kwa kujikita katika: sala, tafakari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kwa uchaji na ibada badala ya kuadhimisha Mafumbo Matakatifu kwa mazoea!

Mapadre wawe wa kwanza kukimbilia na kuiambata huruma ya Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, mambo msingi katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho. Kardinali Stella anakaza kusema, Mapadre wanapaswa kuwa wazi na wakweli mbele ya Mwenyezi Mungu anayewaona kutoka katika undani wa maisha yao, tayari kujipatanisha naye, pale wanapoteleza na kuanguka. Wawe ni moyo wa upendo na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; lakini pia watambue changamoto na hatari wanazoweza kukabiliana nazo katika maisha na utume wao!

Kardinali Stella anapenda kuchukua nafasi hii kuwaangalisha Mapadre kutopenda kukumbatia malimwengu, kwani wanaweza kujikita wanamezwa na kutumbukia na huko watalia na kusaga meno. Mapadre wawe na ujasiri wa kiimani, kwa kujiachilia na kujiaminisha mbele ya Mungu kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha, ili kuwa na mvuto na mashiko ya ushuhuda wa Injili.

Mapadre katika safari ya maisha yao wajitahidi kumwendea Mwenyezi Mungu na kwa njia hii pia wanawaendea binadamu waliokabidhiwa kwao na Kristo pamoja na Kanisa lake. Mapadre wakuze na kudumisha kipaji cha ugunduzi katika shughuli za kichungaji, tayari kumwachia Mungu nafasi ili aweze kuwashangaza. Kamwe, Mapadre wasiwe na shingo ngumu kwani hizi ni dalili za kufilisika kwa maisha ya kiroho na matokeo yake ni kujiundia ngome ya kujilinda.

Ulimwenguni kuna changamoto, matatizo na fursa kibao, Mapadre wasipokuwa makini watajikuta wakijifungia katika ubinafsi wao na kwa kujitafuta wenyewe; mambo ambayo yana athari kubwa katika maisha na imani ya waamini. Padre anayejisadaka na kujitoa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, daima atakuwa na upendo, huruma, imani na matumaini; atakuwa ni chemchemi ya umoja na udugu unaofumbatwa katika kipaji cha ugunduzi wa shughuli za kichungaji. Kwa njia hii, kwa hakika, Kanisa litaweza kuwa ni maabara ya: Matumaini na Unabii; kwa kusaidia kuunda na kufunda dhamiri nyofu; ili kuchuchumilia haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.