2016-12-30 14:04:00

Pd. Maswil ateuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume Jimbo la Kijeshi Kenya


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Alfred Kipkoech Arap Rotich wa Jimbo Katoliki la Kijeshi Nchini Kenya la kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Benjamin Kituto Maswil kuwa ni msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki la Kijeshi nchini Kenya. Itakumbukwa kwamba, Jimbo hili lilianzishwa kunako tarehe 20 Januari 1964 na Hayati Kardinali Maurice Michael Otunga ambaye kwa sasa kuna mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri unaendelea nchini Kenya, ndiye aliyekuwa Askofu wake wa kwanza. Mtumishi wa Mungu Otunga akaliongoza Jimbo hilikuanzia tarehe 20 Januari 1964 hadi tarehe 29 Agosti 1997.

Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa Askofu Afred Kipkoech Arap Rotich kuliongoza Jimbo hili la Kijeshi kuanzia tarehe 29 Agosti 1997 hadi tarehe 30 Desemba 2016 alipong’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Benjamin Kituto Maswil kuwa ni msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Kijeshi nchini Kenya. Jimbo linaundwa ili kusogeza huduma kwa familia ya Mungu katika eneo husika!

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.