2016-12-30 11:13:00

Misimamo mikali ya kidini ni sumu kwa mafungamano ya kijamii


Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Yangon, nchini Myamar anasema, Bara la Asia limebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa dini kuu duniani lakini leo hii, misimamo mikali ya kidini imekuwa ni sumu kali sana katika maisha ya watu wengi Barani Asia. Kardinali Maung Bo ameyasema haya hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa kitabu kijulikanacho kama “On the brink” kilichoandikwa na Padre Michael Kelly, kinachopembua kwa kina na mapana matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo makundi ya dini zenye waamnini wachache Barani Asia.

Kardinali Bo anakaza kusema haki na uhuru wa mtu kuabudu dini anayoitaka kadiri ya dhamiri yake nyofu,  ni tendo takatifu, lakini leo hii, jambo hili limekuwa ni kitendawili kwa nchi nyingi Barani Asia. Watu wanauwawa, wanateswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao hata kwenye nchi ambazo zinajidai kwamba, zinakuza na kudumisha demokrasia. Kuna baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani wanaotishia maisha, usalama pamoja na mafungamano ya kijamii Barani Asia.

Waamini wenye siasa na misimamo mikali ya kidini na kiimani wamekuwa wakipandikiza mbegu ya chuki na uhasama kati ya wananchi na matokeo yake ni vita na machafuko ya kisiasa yanayopelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na wengi wao wa kulazimishwa kuzikimbia nchi zao au kuwa wakimbizi katika taifa lao wenyewe. Wakati mwingine siasa zimechangia kukoleza misimamo mikali ya kidini kwa kuchangia kutunga na kupitisha sheria na sera za kibaguzi. Kardinali Bo anasema, uhuru wa kidini ni jambo muhimu sana ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na mafao ya wengi. Watu wajenge utamaduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe, ni watoto wa Baba mmoja. Tofauti za kidini na kiimani zisiwe ni chanzo cha maafa ya watu na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.