2016-12-29 10:37:00

Askofu mkuu Ruwaichi: Familia ya Kikristo kadiri ya Mwanga wa Injili!


Wosia wa Kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu  familia sanjari na katekesi makini na endelevu zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wote huu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si masuala na changamoto zote za kichungaji na kimaadili zinaweza kutatuliwa kwa njia ya Wosia huu wa kitume licha ya Kanisa kuendelea kujikita katika umoja na utakatifu wa mafundisho yake. Wosia huu unajikita katika Neno la Mungu kwa kuangalia ukweli wa maisha na utume wa familia pamoja na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo.

Hapa kwa namna ya pekee, anagusia tabia ya watu kutopenda kuzaa watoto kutokana na sababu mbali mbali. Waamini kukengeuka na kumezwa mno na malimwengu kiasi hata cha kuweka imani yao rehani; ukosefu wa uhakika wa fursa za ajira na makazi ya watu; tatizo la wakimbizi na wahamiaji, ulemavu na umaskini wa hali na kipato; ndoa za watu wa jinsia moja, bila kusahau dhuluma na nyanyaso dhidi ya wanawake majumbani. Kunachangamoto ambayo imejificha katika ajenda za kimataifa nayo ni usawa wa kijinsia.

Baba Mtakatifu anakazia wito wa familia; umuhimu wa kujenga na kudumisha ndoa pamoja na kuwa ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu Francisko katika wosia wake anapembua kwa kina na mapana changamoto za shughuli za kichungaji kuhusu maisha ya ndoa na familia na kwamba, kuna haja ya kuwajengea uwezo wanandoa ili waweze kujikita zaidi katika malezi na majiundo makini ya watoto wao kwani familia ni Kanisa dogo la nyumbani! Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawasindikiza, wanawasaidia wanandoa kufanya mang’amuzi ya maisha na kuwashirikisha wanandoa wanaoogelea katika kinzani na misigano ya maisha ya ndoa na familia. Mwishoni, Baba Mtakatifu katika wosia wake wa kitume, anawataka wanandoa kujenga na kudumisha tasaufi ya maisha ya ndoa na familia.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika barua yake ya kichungaji kwa familia ya Mungu Jimboni mwake anasema Sakramenti takatifu ya ndoa ni ya msingi kabisa katika Kanisa. Sakramenti hii inahusiana na wito, uwakfu na utume wa mkristo mlei. Wengi katika Kanisa wamepewa wito huu. Wito wa ndoa unamdai mhusika kuzingatia upendo, umoja, uaminifu na udumifu kwa maagano yanayowekwa mbele ya Mungu, mwenzi wa ndoa na Kanisa.

Ukuu na Utakatifu wa ndoa unatokana na ukweli kwamba ndoa yenyewe ni kifungo kitakatifu kati ya mume mmoja na mke mmoja, kifungo alichokianzisha na kukibariki Mungu mwenyewe na Kristo kukipatia hadhi ya kuwa ni Sakramenti ya Kanisa Utume wa ndoa unamdai mwanandoa kuliunda na kulijenga Kanisa la nyumbani yaani familia. Wanandoa wanatekeleza wajibu huu kwa kushirikiana na Mungu katika kazi yake ya uumbaji. Kwa hiyo, wanandoa ni wahudumu wa Injili ya uhai; hilo wanalitekeleza kwa kuwapokea watoto ambao Mungu anapenda kuwajalia na kuwalea kiutu, kiimani, kimaadili na hata kitaaluma.

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema tukubali kwamba Ndoa takatifu ni jambo zito na lenye heshima, mastahili na majukumu mazito. Licha ya kutambua hivyo, bado tunashuhudia kushamiri kwa mwelekeo wa kuchukulia ndoa kiholela na kwa wepesi mkubwa mno. Katika zama hizi, mwelekeo huo unabeba hatari kubwa kwa utakatifu, usitawi na udumifu wa ndoa. Aidha unaathiri utakatifu na uthabiti wa familia, Kanisa la nyumbani. Ili kuikabili changamoto hii, Askofu mkuu Ruwaichi anapenda kutoa maagizo ya kichungaji kama ifuatavyo: Katika kila parokia, iandaliwe na kuundwa timu ya kutoa mafundisho kwa ajili ya wale wanaojiandaa kwa maisha ya ndoa na hata wale ambao wameshafunga ndoa. Timu hizo ziwajumuishe wafuatao: Padre, Mganga au Nesi, Mtaalam wa Sheria, Mtaalam wa maswala ya jamii, katekista na wanandoa (mume na mke) wakomavu na  thabiti. Mafundisho yatolewe na wanajopo wote. Uwekwe muda wa kutosha kwa ajili ya mafundisho hayo.

Iepukwe kabisa tabia ya kupanga mafundisho ya kurashia. Ukuu, utakatifu na umuhimu wa ndoa kama swala la maisha yote linahitaji umakini zaidi. Vijana wanaojitambua kuwa mwelekeo wao ni wa wito wa maisha ya ndoa, wajitahidi kuanza kuhudhuria mafundisho bayana mapema hata kabla hawajaanza habari za uchumba. Hilo litawasaidia kujielewa zaidi, kuyaelewa madai ya ndoa, kuelewa jinsi ya kujipanga kupata mchumba wa kufaa, kujua jinsi ya kujidhibiti na kubandukana na baadhi ya mitazamo na tabia ambavyo haviakisi wito na utakatifu wa ndoa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.