Baba Mtakatifu Francisko amepokea ombi la kustaafu shughuli za kitume kwa Jimbo la Mbalmayo huko Cameroon kutoka kwa Askofu Adalbert Ndzana na kumteua Mheshimiwa Padre Joseph Marie Ndi- Okalla kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki aliyekuwa Gombera wa Chuo Kikuu Katoliki cha Afrika ya Kati (Yaundè) na Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon kwa ajili ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Askofu mteule Joseph Marie Ndi-Okalla alizaliwa 21 Novemba 1957 huko Douala. Baada ya masomo yake ya shule ya msingi aliingia seminari ndogo ya Mbalmayo. Aliendelea na masomo yake ya filosofía kwa mwaka mmoja katika seminari ya Mama yetu Maria mkingiwa wa dhambi ya asili wa Nkolbison, Yaoundé.
Aliendelea na masomo yake ya juu huko Ufaransa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki mjini
Paris na Chuo Kikuu cha Sorbona kwa masomo ya Taalimungu, historia na Mafundisho Jamii
ya Kanisa. Alipata shahada ya uzaminivu katika taalimungu. Jimbo la Mbalmayo liliundwa
mwaka 1961 chini ya Jimbo kuu la Younde lenye wakazi 400,000 kati yao 250 ,000 ni
wakatoliki.Jimbo hilo lina parokia 87 , na linaloshugulikiwa na utume wa mapadre
102 kati yao 77 ni mapadre wa jimbo na 25 mapadre wa mashirika ya kitawa, wapo watawa
wakike 40 na waseminari 66.
Sr Angela Rwezaula.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©. |