2016-12-25 12:09:00

Urbi et Orbi! Kilio cha Baba Mtakatifu kwa ajili ya amani duniani!


Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za Noeli kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake maarufu kama “Urbi et Orbi”, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 25 Desemba 2016 amefafanua kuhusu Fumbo la Umwilisho na kiu ya amani kwa watu wa mataifa yanayoogelea katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kisiasa na kidini, ili watu wote wenye mapenzi mema waweze kushirikiana na kushikamana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anasema, Siku kuu ya Noeli ni mwaliko kwa waamini kushiriki furaha ya Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu pamoja na wachungaji, waliopata fursa ya kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa Mwana wa Mungu kuzaliwa na kulazwa kwenye Pango la kulishia wanyama. Huyu ndiye Yesu, Mkombozi wa dunia. Nabii Isaya anasema, maana kwa ajili yetu Mtoto amezaliwa. Tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa mabegani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele na Mfalme wa amani.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, uweza na nguvu za Mwana wa Mungu si kama za ulimwengu huu zinazokumbatiwa na nguvu na utajiri, bali Yesu ana nguvu ya upendo ulioumba mbingu na dunia; chemchemi ya maisha ya kila kiumbe; ni nguvu yenye mvuto inayowaunganisha bwana na bibi kuwa ni mwili mmoja kwa ajili maisha ya pamoja. Hii ndiyo nguvu ya Mungu inayojikita katika upendo uliomfanya Yesu kuvua utukufu wake na kuwa kama binadamu katika mambo yote isipokuwa na dhambi; akajinyenyekesha, akateswa na kufa Msalabani, siku ya tatu akafufuka kwa wafu!. Hii ni nguvu ya huduma inayojenga na kuimarisha Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika haki na amani duniani.

Ndiyo maana Malaika waliimba “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni na amani kwa watu anaowaridhia. Ujumbe huu anasema Baba Mtakatifu Francisko unapaswa kuwafikia watu wote wa mataifa, hususan wale waliojeruhiwa kwa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; watu wanaotamani kwa nguvu zote amani maisha mwao! Amani kwa wananchi wa Siria ambako damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika hasa huko mjini Aleppo, mahali ambapo kumegeuka kuwa ni uwanja wa vita ya hatari kabisa.

Ni jambo la dharura kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata msaada na faraja, kwa kuzingatia na kuheshimu Sheria na Haki za Kimataifa. Ni muda muafaka kwamba, ngurumo ya silaha isitishwe kabisa na Jumuiya ya Kimataifa itekeleze wajibu wake barabara, ili suluhu ya amani kwa njia ya majadiliano iweze kupatikana ili kuimarisha maridhiano kati ya watu nchini humo!

Amani kwa watu wote wanaoishi katika Nchi Takatifu, iliyochaguliwa tangu awali na Mwenyezi Mungu. Waisraeli na Wapalestina wawe na ujasiri wa kuandika kurasa mpya wa historia yao, kwa kuondokana na chuki pamoja na hali ya kutaka kulipizana kisasi na badala yake, waoneshe utashi wa kujenga kesho iliyo bora zaidi inayojikita katika ushirikiano, uelewano na amani. Baba Mtakatifu anaombea amani na umoja wa kitaifa nchini Iraq, Lybia na Yemen, mahali ambako watu wengi wanateseka kwa vita na vitendo vya kigaidi. Baba Mtakatifu anaombea amani Barani Afrika hususan Nigeria ambako vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kiasi hata cha kuwatumbukiza watoto wadogo katika matukio ya mauaji.

Papa anaombea amani ipatikane nchini Sudan ya Kusini na DRC ili kweli iweze kuganga na kuponya kinzani na mipasuko ya kitaifa, ili kweli watu wote wenye mapenzi mema waweze kushikamana na kuanza hija ya maendeleo na ushirikiano kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utamaduni wa majadiliano na kukataa kishawishi cha mapigano! Baba Mtakatifu anaombea amani huko Ukraine ya Mashariki ili utashi wa pamoja uweze kupatikana na hivyo kuleta nafuu kwa wananchi wasio na hatia sanjari na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana waliyojitwalia.

Baba Mtakatifu anaombea amani nchini Colombia ambayo kwa sasa inataka kuanza tena kwa ujasiri mkubwa safari ya majadiliano na upatanisho. Ujasiri wa namna hii, uwafikie pia wananchi wa Venezuela ili kweli waweze kufanya maamuzi magumu yatakayosaidia kusitisha kinzani ili kwa pamoja waweze kujenga matumaini ya kesho iliyo bora zaidi kwa wote. Baba Mtakatifu anaendelea kutaja litania ya kuombea amani katika maeneo mbali mbali duniani ambamo watu wanateseka kutokana na ukosefu wa haki.

Myanmar inapaswa kuendelea kujizatiti katika amani, utulivu na maridhiano kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa, ili kutoa huduma makini kwa watu wanaohitaji msaada wa dharura. Baba Mtakatifu anaiombea Korea iweze kupita vyema kipindi cha kinzani kwa kujizatiti zaidi na zaidi katika ushirikiano. Amani kwa wale wote waliowapoteza ndugu na jamaa zao kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kupandikiza mbegu ya kifo, woga na wasi wasi kwa watu. Amani imwilishwe katika matendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wanaoteseka kwa baa la njaa na vita.

Baba Mtakatifu Francisko anaombea amani kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na waathirika wa biashara haramu ya binadamu. Amani kwa watu wanaoteseka kutokana na uchu wa mali na madaraka unaofanywa na watu wachache kwa mateso na mahangaiko ya wengi; watu wanaotafuta fedha na mali inayowatumbukiza wengine katika utumwa! Amani kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; matetemeko ya ardhi pamoja na majanga asilia. Amani kwa watoto wote duniani kwa siku hii ambayo Mwenyezi Mungu amejifanya kuwa Mtoto, lakini zaidi kwa watoto ambao hawana tena furaha ya maisha ya utotoni kutokana na baa la njaa, vita na ubinafsi wa watu wazima.

Mwishoni, Baba Mtakatifu ameombea, amani duniani kwa watu anaowaridhia; watu ambao kila siku wanafanya kazi kwa uadilifu na uvumilivu mkubwa, katika familia na jamii katika ujumla wake ili kujenga dunia inayojikita katika utu, haki pamoja na kutambua kwamba ni kwa njia ya amani kuna uwezekano wa kesho na maendeleo pamoja na ustawi wa wote. Yesu Kristo aliyezaliwa ni Mfalme wa amani, mwaliko kwa wote kumpokea. Baada ya baraka kuu ya Noeli, Baba Mtakatifu Francisko aliwatakia watu wote heri na baraka za Noel ina kwamba, wanaalikwa kumtafakari Mtoto Yesu anayewakirimia walimwengu amani, changamoto ya kumwilsiha matumaini kwa njia ya ushuhuda wa mshikamano na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.