2016-12-25 12:26:00

Mtoto aliyezaliwa ni Mfalme wa amani, furaha na ukweli wa maisha


Mtakatifu Paulo anasema, maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa katika mkesha wa Noeli kwa kuwajalia zawadi kubwa ya Mtoto aliyezaliwa, kielelezo makini cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni usiku wa utukufu wa Mungu unaoimbwa na kutangazwa na Malaika, kwa uwepo wa daima wa Mungu kati ya watu wake, kwani amefanyika mwili na kukaa kati yao. Huu ni usiku wa mwanga unaowaangazia wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti; ni utukufu wa Bwana uliowang’aria wachungaji waliokuwa Bethlehemu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha wa Noeli, tarehe 24 Desemba 2016 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, wachungaji walimwona Mtoto mchanga aliyezaliwa kwa ajili ya binadamu, wakashuhudia utukufu, furaha na mwanga uliooneshwa na Malaika. Mtoto Yesu aliyelazwa katika hori ya kulishia wanyama ni alama makini na endelevu inayowawezesha waamini kumwona Yesu. Maadhimisho ya kweli ya Siku kuu ya Noeli yanafumbatwa katika tafakari ya uwepo wa Mungu kwa njia ya alama ya mtoto mchanga; mpole aliyelazwa na kufunikwa kwa upendo.

Baba Mtakatifu anasema, Injili inafunua kinyume chake kwa kuwaonesha viongozi wakuu na watu mashuhuri wa nyakati zile, lakini kwa bahati mbaya Mwenyezi Mungu hakuwepo huko; wala hakujifunua katika majumba ya kifahari, lakini amejifunua katika hali ya umaskini kwenye hori ya kulishia wanyama, katika hali ya kawaida kabisa ya maisha pasi na majigambo! Bila vitisho na nguvu, bali katika udogo unaoshangaza.

Ili kuonana na Mwenyezi Mungu kuna haja ya kumwendea huko aliko ili kumpigia magoti na kujinyenyekesha kama mtoto mdogo, kwani Mtoto aliyezaliwa anawachangamotisha waamini kuondokana na mawazo ya kufikirika, ili kuambata mambo msingi; kuachana na tabia ya madai yasiyotoshelezwa, hali ya kutoridhika pamoja na majonzi ya daima pale wanapokosa hata mambo madogo madogo. Haya ni mambo yanayopaswa kuwekwa pembeni ili kukutana na Mwenyezi Mungu aliyejifanya kuwa Mtoto wa amani, furaha na maana ya kweli ya maisha!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari hatima ya watoto wanaoteseka kwa kukosa upendo na faraja kutoka kwa wazazi wao; watoto wanaokosa “hori ya utu na heshima ya binadamu” ili kupata mahali pa kujificha dhidi ya mabomu; mazingira magumu na hatarishi mijini; pamoja na mashua zinazofurika wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Ni watoto wanaokumbana na ukatili kwa kufutiliwa mbali hata kabla ya kuzaliwa; watoto wanaolalama kwa njaa, kiu na magonjwa lakini hakuna anayethubutu kutuliza njaa yao; hawa ni watoto ambao badala ya kupewa michezo ya watoto, wanabebeshwa silaha za mahangamizi!

Baba Mtakatifu anasema, Fumbo la Umwilisho linajikita katika matumaini na majonzi, pale ambapo Injili ya uhai inapotemwa na kutupiliwa mbali, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, ambao hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Yesu anazaliwa katika mazingira ya kukataliwa na kutengwa na watu, kama inavyojitokeza hata wakati huu, badala ya Kristo Yesu kuwa ni kiini cha Noeli, baadhi ya watu wanajipatia umaarufu, kwa mwanga wa shughuli za biashara unaofifisha mwanga wa Mungu; kwa kupeana zawadi za Noeli na kuwasahau maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Fumbo la Umwilisho kimsingi linaambata cheche za matumaini licha ya giza la maisha ya mwanadamu, lakini mwanga wa Mungu unang’ara zaidi, bila kuogofya, kwani Mungu anapenda kuwavuta watu kwake; anataka kugeuka kuwa ni mkate kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele pamoja na kuwashirikisha upendo wake usiokuwa na kifani. Ni Mungu anayekuja kulisha na kuhudumia, kielelezo makini kinachojionesha hata katika Fumbo la Pasaka, Yesu atakapogeuka kuwa ni mkate utakaomegwa, ushuhuda wa upendo unaojisadaka na kuokoa; upendo unaotoa mwanga wa maisha na amani katika nyoyo za watu!

Wachungaji kondeni ambao walikuwa si mali kitu kwa wakati ule, ndiyo watu waliobahatika kualikwa na hatimaye, kulifahamu Fumbo la Umwilisho, mwaliko kwa waamini kumwendea Yesu kwa imani na matumaini; kwa kutambua mapungufu yao, ili aweze kuwagusa kwa upendo wake unaookoa; wajenge ujirani mwema na Mwenyezi Mungu ambaye ameamua kuwa kati pamoja nao. Pango la Mtoto Yesu wakati wa Noeli liwakumbushe waamini: mwanga na amani; muhtasari wa umaskini na hali ya kukataliwa.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni changamoto ya kumwendea Yesu jinsi walivyo: kwa kumwonesha madonda yao ambayo hayajapona na kwa njia hii, wataweza kuliishi kikamilifu Fumbo la Umwilisho, kwa kugundua uzuri wa kupendwa na kuthaminiwa na Mungu, kwani Yesu anazaliwa kama mkate wa maisha ya uzima wa milele, kielelezo cha upendo mnyofu na usiokuwa na kifani! Ni nafasi ya kumshukuru Yesu aliyefanya yote haya kwa ajili yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.