2016-12-24 10:51:00

Askofu Desfarges ateuliwa kuwa Askofu mkuu Jimbo kuu la Alger


Baba Mtakatifu Francisko amemtea Askofu Paul Desfarges, S.J. kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Alger, nchini Algeria. Hadi kuteuliwa kwake Askofu mkuu mteule Paul Desfarges alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Costantine nchini Algeria. Alizaliwa tarehe 7 Mei 1944 huko Saint-Etienne, Ufaransa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi kunako mwaka 1967 akajiunga na Shirika la Wayesuit. Akajiendeleza kwa masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Nice ambako alijipatia Shahada ya Uzamivu katika masomo ya Saikolojia.

Tarehe 14 Juni 1975 akapewa Daraja ya Upadre na kuweka nadhiri za daima kunako tarehe 30 Aprili 1981. Kunako mwaka 1976 alitumwa kwenda Jimbo Katoliki la Costantine kama Jaalim wa Saikolojia katika lugha ya Kiarabu katika Chuo kikuu mahalia. Kuanzia mwaka 1983 hadi mwaka 2005 alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo Katoliki Costantine sanjari na kuendelea kufundisha hadi mwaka 2006. Alikuwa ni Mkuu wa Shirika la Wayesuit hadi alipoteuliwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Costantine kunako tarehe 21 Novemba 2008 na kuwekwa wakfu mwezi Januari 2009. Kuanzia tarehe 23 Mei 2015 Askofu mkuu mteule Paul Desfarges alikuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Alger baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumteua Askofu mkuu Ghaleb Abdalla Bader kuwa Balozi wa Vatican nchini Pakistan.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.