2016-12-23 11:52:00

Ufukara ni mama na nguzo ya maisha na utume wa Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amemwandikia barua ya shukrani Padre Juliàn Carròn, Rais wa Jumuiya ya Udugu wa Umoja na Uhuru kwa sadaka waliyomkirimia baada ya hija zao za maisha ya kiroho, ili kuchangia huduma ya matendo ya huruma inayotekelezwa na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake! Anawapongeza wanachama wake ambao wamefanya hija kwenye Madhabahu zaidi mia mbili nchini Italia na sehemu mbali mbali za dunia; wengi wao wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu wamefanya hija ya huruma ya Mungu rohoni mwao kwa kujinyima, ili kuwaonjesha wengine ukarimu unaofumbatwa katika maisha ya Kikristo!

Baba Mtakatifu katika barua hii anasema, maskini ni amana na hazina ya Kanisa. Maskini wanalihamasisha Kanisa kujikita katika mambo msingi ya maisha na utume wake. Changamoto hapa si kugawa mali kwa ajili ya maskini peke yake kama anavyosema Mtakatifu Augustino, bali ni kuanzisha mchakato wa kuwa fukara mbele ya Mungu, ili kuonesha kwamba, kweli waamini hawa wana kiu ya uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Huduma kwa maskini, iwasaidie kumgundua Kristo Yesu aliyekuwa fukara kwa ajili ya binadamu.

Mtakatifu Ignasi wa Loyola anakaza kusema, ufukara ni mama na ukuta! Ni mama kwani una uwezo wa kuzalisha maisha mapya ya kiroho; yanayojikita katika utakatifu na utume mkamilifu. Ufukara ni ukuta kwani ni ngao inayolinda maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kumekuwepo na kashfa na majanga mengi katika maisha na utume wa Kanisa pale ambapo, ufukara haukupewa kipaumbele cha pekee na Mama Kanisa.

Kwa bahati mbaya, ulimwengu mamboleo umejikita katika mantiki ya kutafuta faida kubwa kwa gharama yoyote ile na matokeo yake ni kuzaliwa kwa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Kutokana na mwelekeo huu, Baba Mtakatifu anakaza kusema, anatamani kuona Kanisa maskini kwa ajili maskini, kwani kwa njia hii, Kanisa litaweza kurejea tena katika mambo msingi ya maisha na utume wake, si kwa kukumbatia ya kale, bali kujichotea nguvu ya mwanzo mpya wa ujasiri kuelekea kesho iliyo bora zaidi, yaani mageuzi ya wema na upendo wa Mungu kwa binadamu! Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaomba wanachama wa Jumuiya ya Udugu wa Umoja na Uhuru kuungana naye katika nia hii njema ili kuweza kufikia lengo linalokusudiwa. Anawataka waendelee kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa amani na utulivu sanjari na ushuhuda unaosimikwa katika ujasiri na uhakika wa maisha ya Kikristo!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.