2016-12-23 11:35:00

Noeli: Yesu azaliwe mioyoni mwenu!


Aliyetungwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu akazaliwa na Bikira Maria ndiyo tema iliyochambuliwa na Padre Raniero Cantalamessa Ijumaa, tarehe 23 Desemba 2016 wakati wa mahubiri yake ya nne ya Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2016 yanayoongozwa na kauli mbiu “Roho Mtakatifu ni chemchemi ya matumaini. Mahubiri haya yamehudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, viongozi wakuu wa Sekretarieti ya Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwenye Kikanisa cha “Mama wa Mkombozi” “Redemptoris Mater” kilichoko mjini Vatican.

Kwa ufupi, Padre Cantalamessa amejikita zaidi katika Siku kuu ya Noeli, Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya binadamu, kazi iliyofanywa na Roho Mtakatifu, Bikira Maria akawa ni Mama wa Mungu, yaani “Theotokos” na Yesu akazaliwa kwa ajili ya ukombozi wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yesu Kristo alizaliwa wakati wa Sensa ya Watu, hali inayoonesha pilika pilika kwa wakati ule na kwamba, wahusika wakuu katika mazingira haya ni Mfalme Cesare Augusto, Erode, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Mazingira haya ya maisha ya kiroho yanajirudia tena kila mwaka wakati wa Siku kuu ya Noeli.

Hata leo huu kuna vitendo vya kigaidi, vita na majanga mbali mbali ambayo yanawalazimisha watu kuyahama makazi yao kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Katika msongamano wa watu mjini Bethlehemu, Maria na Yosefu hawakubahatika kupata nafasi katika nyumba ya wageni, shida na mahangaiko yote ya siku ile, akayahifadhi katika sakafu ya moyo wake kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Hii inaonesha kwamba, Fumbo la Umwilisho ni kwa ajili ya wokovu wa binadamu ndiyo maana Mtakatifu Augostino anasema, haya ni maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho linalopaswa kufafanuliwa maana yake, ili liweze kupokelewa katika utakatifu wa maisha.

Noeli ni maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, Papa Leo mkuu anasema, hii ni Sakramenti ya kuzaliwa kwa Kristo inayowapatia fursa Wakristo kuzaliwa na Kristo kama ilivyo pia wanapokufa na kufufuka na Kristo kwa kufia dhambi. Maria ni Bikira na Mama wa Kanisa, Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyezaliwa kwa njia ya Roho Mtakatifu, kielelezo makini cha uaminifu wake. Ni mfano bora wa Kanisa linalopaswa kuiga utakatifu, imani, ubikira na umama wake na waamini wanapoiga fadhila za Bikira Maria wanaweza kusaidia mchakato wa kuzaliwa na kukua kwa Yesu Kristo mioyoni mwao.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, Bikira Maria alitunga mimba kwa njia ya Roho Mtakatifu, kumbe, Roho Mtakatifu pia ni Muumbaji anasema Mtakatifu Ambrose kwani ni Bwana mleta uzima! Roho Mtakatifu kwa Bikira Maria anakuwa chemchemi hai ya maji ya uzima, moto wa upendo kwa kupakwa mafuta ya maisha ya kiroho. Hii ni barua ya Kristo iliyoandikwa la Roho Mtakatifu katika nyoyo za watu. Roho Mtakatifu alimwezesha Bikira Maria kuwa na upendo wa Kristo hata kabla ya Kristo Yesu kuzaliwa.

Fumbo la Umwilisho kwa Bikira Maria limekuwa ni tukio la bidii ya maisha ya kiroho, mwanzo wa Pentekoste katika maisha yake. Bikira Maria anapomtembelea Elizabeth anashuhudia upendo, furaha, amani na mwanga wa maisha ya kiroho kwani alikuwa ameyachota yote haya kutoka kwa Roho Mtakatifu kama anavyoshuhudia kwa hali ya unyenyekevu katika Utenzi wake wa “Magnificat”. Maria hata baada ya kuambiwa kwamba atakuwa ni Mama wa Mungu, aliendelea kubaki mnyenyekevu na mtu wa kiasi kana  kwamba, hakuna jambo lolote kubwa ambalo limetokea katika maisha yake. Alithubutu kufuatana na watu wengine ili kumwona Yesu katika maisha na utume wake.

Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Tabernakulo” ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Kumbe, Yesu ni mzao mbarikiwa wa Tumbo la Bikira Maria, ndiyo maana Origeni kunako karne ya tatu akamwita Bikira Maria, Mama wa Mungu, yaani “Theotokos”. Hapa Mababa wa Kanisa wakakiri kwamba, “Ni Mungu kweli na Mtu kweli”, aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye Umungu mmoja sawa na Baba! “Theotokos” ni kielelezo cha utakatifu, imani na Ibada ya Kanisa kwa Bikira Maria aliyekuwa na imani thabiti kiasi hata cha kuweza kumwona Mwanaye wa pekee, akiinamisha kichwa na kukata roho.

Bikira Maria anasema Mtakatifu Augostino ni Mama wa Imani, kwani alimwamini Neno wa Mungu na kumwilisha mafundisho yake katika hija ya maisha yake. Akawa mwanafunzi mwaminifu na Mama wa Kristo mambo yanayofumbatwa katika “utakatifu wote wa Bikira Maria” “Panhagia”. Mababa wa Kanisa wanasema, Yesu anapaswa kuzaliwa katika roho na nyoyo za waamini. Mtakatifu Tomasi wa Akwino anasema “Neno wa Mungu alizaliwa kwa Baba tangu milele yote; Akazaliwa na Bikira Maria hapa duniani na mwishoni anapaswa kuzaliwa katika roho na nyoyo za waamini, muujiza ambao Mtakatifu Yohane XXIII aliomba kwa Yesu kuzaliwa tena upya katika maisha ya waamini.

Siku kuu ya Noeli licha ya kupambwa na mambo mengi ya nje, inapaswa kuwa ni sehemu ya mchakato wa upyaisho wa maisha ya kiroho ili waamini waweze kuungana na Bikira Maria kwa kusema “Ndiwe mwanangu mimi leo nimekuzaa”. Yesu mwenyewe anatamani kuzaliwa katika nyoyo za waja wake. Yesu Kristo, Mwana wa Baba wa milele, aliyetungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu alizaliwa mjini Bethlehemu na huo ukawa ni mwanzo mpya wa historia na matukio mbali mbali katika maisha ya mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.