2016-12-23 13:49:00

Mkesha wa Siku kuu ya Noeli mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Mkesha wa Noeli kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 24 Desemba 2016 kuanzia saa 3:30 kwa Saa za Ulaya. Tarehe 25 Desemba 2016, Siku kuu ya Noeli, Baba Mtakatifu atatoa Salam za Noeli kwa Mji wa Roma na Dunia kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini “Urbi et Orbi”.

Wakati wa mkesha wa Noeli, Kanisa litakapokuwa linaimba Utukufu kwa Mungu juu mbinguni na amani duniani kwa watu anaowaridhia, Sanam ya Mtoto Yesu itapelekwa kwenye Pango la Noeli, lilowekwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na Maafisa wa Kikosi cha Zima moto na Afisa kutoka katika Vikosi vya ulinzi na Usalama vya Vatican. Kanisa linapenda kutambua na kuenzi mchango wa askari katika huduma ya ulinzi, usalama na uokoaji unaotekelezwa na vikosi vya ulinzi na usalama wakati wa majanga mbali mbali, kama ilivyojidhihirisha hivi karibuni wakati wa tetemeko la ardhi Kati kati ya mwa Italia.

Wanajeshi wamekuwa bega kwa bega katika maisha na watu walioguswa na kutiswa na tetemeko la ardhi, kiasi kwamba, wao kweli wamekuwa ni tumaini na kimbilio lao wakati shida na mahangaiko ya ndani! Walipotaka kurejea kwenye magofu na mahame yao, wanajeshi hawa wamekuwa ni dira na mwongozo wa kufuata. Hii ni kazi na huduma inayotekelezwa katika hali ya unyenyekevu, weledi na sadaka kubwa ndiyo maana wakati wa Mkesha wa Noeli, Kanisa linawakumbuka na kuwapongeza kwa kazi na utume uliotukuka unaotekelezwa na mashujaa hawa miongoni mwa wananchi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.