2016-12-21 09:23:00

Ujerumani endeleeni kuonesha mshikamano wa kijamii!


Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Tume Mabaraza ya Maaskofu kwenye Umoja wa Ulaya, COMECE ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani anasema, amesikitishwa sana na shambulizi la kigaidi lililotokea Jumatatu tarehe 19 Desemba 2016 kwenye Soko la Noeli huko Ujerumani. Anaialika familia ya Mungu nchini Ujerumani kuendelea kushikamana katika umoja na udugu. Shambulizi hili ni kinyume kabisa cha matarajio ya wengi kwenye Soko la Noeli huko Ujerumani.

Kardinali Marx anapenda kuchukua nafasi hii kutuma salam zake za rambi rambi kwa wale wote waliofikwa na msiba huu mzito wa kuondokewa na ndugu, jamaa na rafiki zao, anawaombea majeruhi kupona haraka ili waweze kurejea tena katika shughuli zao za kila siku. Kardinali Reinhard Marx anasema, katika kipindi hiki kigumu, wanapaswa kushikamana kama jamii na wala wasikubali vitendo hivi vya kigaidi viwavuruge na kuwasambaratisha!

Viongozi mbali mbali kutoka Jumuiya ya Kimataifa wamelaani kwa ukali mashambulizi haya ya kigaidi yaliyopelekea watu 12 kupoteza maisha na wengine 48 kujeruhiwa vibaya. Wameonesha mshikamano wao na  wananchi wa Ujerumani katika kipindi hiki kigumu pamoja na kuwatumia salam za rambi rambi. Ulinzi na usalama unaendelea kuimarishwa Barani Ulaya hasa Kipindi hiki cha Noeli na shamra shamra za Mwaka Mpya 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.