2016-12-21 08:40:00

Kanisa limejizatiti kudumisha majadiliano ya kidini!


Kardinali Jean Lous Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, Kanisa litaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, maridhiano na ushirikiano kati ya watu na kwamba, mashambulizi pamoja na vitendo vya kigaidi, kamwe visiwe ni kikwazo cha majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia majadiliano ya matumaini kati ya waamini wa dini mbali mbali ili kweli dini ziweze kuwa ni kikolezo cha amani, upendo na maridhiano kati ya watu.

Kardinali Tauran anasema, mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika nchini Ujerumani, Misri, Ufaransa na Ubelgiji pamoja na maeneo mengine ya dunia yanaendelea kuzua hofu na mashaka makubwa, lakini kamwe hayawezi kulikatisha Kanisa tamaa ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini. Mauaji ya Padre Jacques Hamel nchini Ufaransa yaliibua mshikamano wa umoja, upendo na udugu miongoni mwa familia ya Mungu nchini Ufaransa.

Bado kuna changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, yaani wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi Barani Ulaya; athari za mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa; vita, dhuluma na nyanyaso huko Siria na Mashariki ya Kati. Mambo yote haya yanahitaji majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, amani na maendeleo ya wengi. Haya ni majadiliano yanayopaswa pia kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kila siku ya maisha! Watu wanapaswa kuondokana na tabia ya kutaka kujichukulia sheria mkononi, kwa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu; kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta haki na amani, ili kudumisha umoja na udugu hata katika tofauti msingi za kidini na kiimani! Kufanya hija, kusali na kufunga ni mambo ya kawaida yanayoweza kusaidia kukoleza mchakato wa haki, amani na mafungamano ya kijamii.

Mwaka 2016 umekuwa na mafanikio makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kwani tarehe 23 Mei 2016, Baba Mtakatifu alibahatika kukutana na kuzungumza na Imam mkuu wa Al-Azhar, Sheikh mkuu Ahmad Muhammad Al Tayyib pamoja na ujumbe wake. Viongozi hawa walikazia umuhimu wa waamini wa dini zao kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano, kwa kukataa kishawishi cha kutumia dini kama chanzo cha vita, kinzani na vitendo vya kigaidi duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kwamba, hakuna dini yoyote duniani inayohalalisha vita, dhuluma na nyanyaso kwa watu. Waamini wanapofanya vitendo hivi vyote ni kufuru dhidi ya Mungu na dini zao. Misimamo mikali ya kidini na kiimani ni hatari kwa maisha, utu na heshima ya binadamu. Huruma na upendo wa Mungu ni mambo msingi yanayowaambata na kuwasindikiza waamini katika safari ya maisha yao hapa duniani. Wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wa dini mbali mbali waliweza kushiriki tukio hili la maisha na utume wa Kanisa kwani upendo na huruma ya Mungu haina ubaguzi kwa mtu awaye yote!

Ni matumaini ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwamba, Mwaka 2017 utaendeleza majadiliano na Chuo Kikuu cha Kiislam cha Cairo. Viongozi wakuu wa Baraza wameshiriki katika matukio ya kimataifa yaliyopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya waamini wa dini mbali mbali kama ilivyotokea mwanzo mwa Mwaka 2016 pamoja na kushiriki katika mkutano mkuu wa Wasomi wa Kiarabu uliofanyika huko Abu Dhabi. Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwaka 2016 amepata pia fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa dini mbali mbali duniani, hali ambayo inasaidia kukuza na kudumisha mchakato wa umoja na udugu kati ya waamini wa dini mbali mbali. Majadiliano ya kidini, ushirikiano, umoja na udugu ni mambo ambayo yanaendelea kupewa uzito wa pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya majadiliano ya kidini.

Baraza pia limekuwa likitoa ujumbe wa matashi mema kwa waamini wa dini mbali mbali wakati wa maadhimisho ya Siku kuu muhimu  kama Deepavali kwa Wabudha na baada ya Mfungo wa Mwezi Mkutukufu wa Ramadhan kwa waamini wa dini ya Kiislam. Baba Mtakatifu Francisko amepata pia fursa ya kusali pamoja na viongozi mbali mbali wa kidini ili kuombea amani duniani kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II mjini Assisi kunako mwaka 1986 kama sehemu ya mwendelezo wa changamoto ya majadiliano ya kidini iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kuzima kiu ya amani na kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.