2016-12-21 13:56:00

DRC: simameni kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi!


Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 21 Desemba 2016 kwenye Ukumbi wa Paulo VI ulioko mjini Vatican, amewataka wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujikita katika majadiliano kwa njia ya amani na utulivu hasa katika kipindi hiki kigumu cha mpito katika historia ya nchi yao. Kwa hakika anawataka wananchi wote wawe ni wasanii wa upatanisho na amani.

Baba Mtakatifu anasema, anapenda kurudia ombi hili kutokana na mazungumzo mazito aliyofanya na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki kutoka nchini DRC waliomtembelea hivi karibuni mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawataka wale wote wenye dhamana ya uongozi nchini DRC kusikiliza sauti ya dhamiri zao nyofu, wawe na ujasiri wa kuona mateso na mahangaiko ya wananchi wenzao, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anapenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia wananchi wote wa DRC upendo na uwepo wake wa karibu na kuwataka wote kujiaminisha katika Mwanga wa Mkombozi wa Ulimwengu. Baba Mtakatifu anawaombea ili kweli Noeli ya kuzaliwa kwa Mkombozi Yesu Kristo, iweze kuwafungulia njia ya matumaini. Taarifa kutoka DRC zinaonesha kwamba, tayari watu watatui wamekwishafariki dunia kutokana na hali tete inayoendelea nchini DRC kwa upande wa upinzani ukimtaka Rais Josefu Kabila kung’atuka kutoka madarakani baada ya muda wake Kikatiba kumalizika rasmi hapo tarehe 19 Desemba 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.