2016-12-20 09:31:00

Simameni kidete ili kweli Mwaka 2017 uwe ni Mwaka wa Amani


Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Yangon nchini Myanmar, anawaalika viongozi wa dini na makabila mbali mbali nchini humo ili kuunganisha nguvu zao, ili hatimaye, kusimama kidete kuhakikisha kwamba, mwaka 2017 unakuwa kweli ni Mwaka wa Amani nchini humo. Amani ya kweli inaweza kupatikana kwa kujikita katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili, kama anavyokaza kusema, Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa kitume: “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”. Haya ni mambo yanayofumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi.

Kardinali Charles Maung Bo anawaalika waamini wa dini na makabila mbali mbali nchini humo, kujitokeza kwa wingi hapo tarehe Mosi, Januari 2017 ili kuombea amani, inayopaswa pia kumwilishwa katika matendo. Hii itakuwa ni siku ya sala na kufunga kwa ajili ya kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia zawadi ya amani ambayo inapaswa kudumisha na wote kwa kuondokana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Sala na kufunga ziwasaidie watu kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuachana na matendo ya giza, ili kweli Mwaka 2017 uwe ni Mwaka wa Amani.

Kardinali Charles Maung Bo anasema, maadhimisho ya Mwaka Mpya iwe ni fursa ya kujikita katika kulinda, kujenga na kudumisha utamaduni wa amani kwani hakuna furaha ya kweli wakati kuna vita inaendelea kurindima sehemu mbali mbali za Myanmar. Hakuna furaha ya kweli wakati bado kuna watu zaidi ya laki mbili wako kwenye kambi za wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kuna nchi kama Cambodia na Vietnam ziliweza kumaliza vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na sasa nchi hizi ziko kwenye hija ya amani na maendeleo endelevu.

Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, Myanmar bado watu wanatwangana kwa vita. Hali hii inaonesha mateso na mahangaiko ya wananchi wengi wa Myanmar. Watu wako kimya, lakini wanateseka sana, kumbe, umefika wakati wa kuunganisha nguvu kwa kuweka pembeni silaha, ili amani, haki, upendo na mshikamano wa kitaifa vianze kutawala tena katika akili na nyoyo za watu! Amani ya kweli ni chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.