2016-12-20 15:00:00

Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kigaidi huko Ujerumani


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na kitendo cha kigaidi ambacho kimepelekea watu 12 kupoteza maisha na wengine 48 kujeruhiwa vibaya huko Berlin, nchini Ujerumani, Jumatatu usiku tarehe 19 Desemba 2016. Katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Heiner Koch, Baba Mtakatifu anasema, yuko karibu na wote walioguswa na kutikiswa na kitendo hiki cha kigaidi na kwamba, anaungana nao kwa ajili ya kuwaombea wale walipofariki dunia, ili waweze kuonja huruma ya Mungu; majeruhi waweze kupona haraka na kuendelea na shughuli zao.

Baba Mtakatifu anavishukuru na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama nchini Ujerumani kwa kazi kubwa wanayoendelea kufanya. Baba Mtakatifu anaungana na watu wote wenye mapenzi mema kulaani vitendo vya kigaidi na kwamba, kamwe visipewe nafasi duniani. Baba Mtakatifu anawaombea wote huruma ya Baba wa mbinguni, faraja, ulinzi na baraka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.