2016-12-20 11:46:00

Dr. Barbara Jatta ateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Makumbusho ya Vatican


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Dr. Barbara Jatta kuwa mkurugenzi mkuu mpya wa Makumbusho ya Vatican, uteuzi unaoanza rasmi tarehe Mosi, Januari 2017. Hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Mkurugenzi msaidizi wa Makumbusho ya Vatican. Dr. Jatta alizaliwa tarehe 6 Oktoba 1962 mjini Roma. Kunako mwaka 1986 alijipatia shahada ya Uzamivu katika Fasihi kutoka Chuo Kikuu cha “La Sapienza” kilichoko mjini Roma. Baadaye alijiendeleza katika masomo ya utunzaji wa nyaraka kutoka katika Shule ya Vatican na hatimaye, kujipatia shahada.

Kunako mwaka 1991 alijiendeleza zaidi katika fani ya “Historia ya Sanaa” kutoka kwenye Chuo kikuu cha Roma. Akajiendeleza zaidi katika masomo haya kwa kuandika na kuchapisha makala mbali mbali kwa ajili ya Sanaa za Maonesho. Kuanzia Mwaka 1994 alipata nafasi ya kufundisha “Historia ya Sanaa” huko Napoli. Kunako mwaka 1996 akafanikiwa kupata nafasi ya kufanya kazi katika Maktaba kuu ya Kitume ya Kanisa Katoliki mjini Vatican.

Akadhaminishwa kuwa ni mkuu wa kitengo cha habari hadi mwaka 2010 kama mhariri mkuu wa Idara ya Michoro. Mwezi Juni, 2016 akahamishwa kutoka katika Maktaba kuu ya Kitume ya Kanisa Katoliki mjini Vatican na kupelekwa kuwa Mkurugenzi mkuu msaidizi wa Makumbusho ya Vatican, hadi kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 20 Desemba 2016 kuwa Mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.