2016-12-19 14:02:00

Siku ya Wahamiaji Kimataifa, vifo zaidi ya 7189


Takribani wahamiaji 7,189 wamefariki dunia kwa mwaka 2016, ambapo zaidi ya nusu ya hesabu hiyo wamefariki ndani ya bahari ya Mediterania. Takwimu hizi zimetolewa na Shirika la Kimataifa la Wahamaji kwa siku ya Wahamiaji duniani, iliyowekwa na Umoja wa Mataifa kuwa tarehe 18 Disemba kila mwaka. Bwana Ban Ki-moon, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewaalika viongozi wa serikali duniani kote kuzingatia hatua zilizokubaliwa mwezi Septemba 2016 juu ya wahamiaji, ili kuepuka ongezeko la wimbi kubwa la watu wanaolazimika kuhama makazi yao.

Inasikitisha kuona kwamba kila siku kuna wastani wa wahamiaji 20 wanaofariki sehemu mbali mbali dunaini. Takwimu za mwaka 2014 ni wahamiaji 5,267 waliofariki dunia katika mahangaiko mbali mbali sehemu tofauti tofauti duniani, na kwa mwaka 2015 idadi ilipanda kufikia wahamiaji 5,740. Wakati mwaka 2016 haujafikia mwisho, tayari kunaonekana ongezeko la vifo vya zaidi ya wahamiaji 1000 kulinganisha na mwaka uliopita wa 2015. Vifo hivi kwa asilimia kubwa vinatokea maeneo ya Bahari ya Mediterania, Afrika magharibi, Afrika ya kati, katikati mwa Amerika ya kusini na kwenye mpaka kati ya Marekani na Mexico.

Ban Ki-moon, katika maadhimisho ya siku ya wahamiaji duniani amesema: dunia imeshashuhudia athari endelevu za kinzani na mapigano ya silaha kati ya watu, vifo, uharibifu na kutangatanga kwa raia. Dunia imeshuhudia pia baadhi ya vikundi na sera zinazowanyanyapaa na kuwafukuzia mbali wahamiaji ikiwa ni pamoja na kuwashutumu kwa makosa mengi katika jamii zao. Ban Ki-moon kawaalika wanadamu wote kuzingatia kuwa wahamiaji ni wanadamu wenye haki zao na wanaostahili kuheshimiwa utu wao. Kwa sababu hiyo amewaalika viongozi wa nchi asilia za wahamiaji, nchi wanamopita na nchi wanakokwenda kuishia, kuweka ushirikiano wa kutosha kukabiliana na changamoto ya wimbi la wahamiaji.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.