2016-12-19 12:03:00

Papa awataka vijana kuwa ni chemchemi ya furaha na amani kwa jirani zao


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 19 Desemba 2016 amekutana na kuzungumza na Vijana Wakatoliki Italia kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana heri na baraka kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli. “Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea Habari Njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi ndiye Kristo Bwana. Kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni chemcghemi ya furaha inayomwezesha mwanadamu kugundua kwamba, anapendwa na Mungu na kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ameamua kuja kukaa pamoja nao, ili kuwaokomboa.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana hawa kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu hata pale wanapokuwa na huzuni moyoni au pale mambo yanapoonekana kwenda mrama! Au wanaposalitiwa na marafiki zao au kujisaliti wenyewe kwani yote mawili yanawezekana kabisa! Lakini, watambue daima kwamba, Mungu anawapenda, kamwe hawezi kuwaacha wala kuwatelekeza, kwani Mungu daima ni mwaminifu kwa ahadi zake na anaendelea kufuata nyayo za watu wake, hata pale wanapokengeuka na kutokomea katika dhambi na uvuli wa mauti. Upendo wa Mungu unamwezesha Mkristo kuwa ni chemchemi ya furaha!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutambua kwamba, furaha hii ni zawadi inayopaswa kutolewa ushuhuda kwa njia ya mahusiano na mafungamano katika familia, shule, parokia na sehemu mbali mbali za maisha yao. Anawashukuru kwa kuendelea kufundwa na kwamba, kauli mbiu ya mwaka 2016 ni “Mmezungukwa na furaha”, kielelezo cha umoja na udugu, furaha na maisha kama wasafiri wanaojisikia kuwa kweli ni sehemu ya Jumuiya ya Kikristo inayojipenyeza katika uhalisia wa maisha ya kimissionari yanayosambaa na kuenea sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwashirikisha furaha ya kweli wale wote wanaokutana nao katika safari ya maisha.

Vijana hawa wanapaswa kutangaza na kushuhudia upendo na wema wa Kristo, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni mitume wa Furaha ya Injili inayowaambata pia jirani zao. Lakini, furaha hii kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawataka kuwashirikisha mababu na mabibi zao huko nyumbani, kwani wao wamekuwa ni chimbuko la ujuzi na maarifa kutokana na maswali kemkem wanayowauliza kila siku. Wazee wanayo kumbu kumbu ya historia na maisha, kumbe, wanaweza kuwa ni zawadi kubwa ambayo itawasaidia katika hija ya maisha yao.

Wazee wana hamu ya kuwasikiliza ili kutambua matarajio na matumaini yao kwa siku za usoni. Vijana hawa wajenge utamaduni wa kuwasikiliza wazee kwani wao wana hekima ya maisha! Vijana wajizatiti katika kukuza amani na mshikamano kwa vijana wenzao ambao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi huko Napoli. Hii ni njia muafaka inayoonesha ni kwa jinsi gani vijana hawa wanataka kutangaza na kushuhudia Uso wa upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu mwishoni, amewashukuru walezi na wasaidizi wao kwa majitoleo yao yanayowasaidia vijana kufundwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo. Amewatakia heri na baraka ya Noeli kwao wenyewe pamoja na familia zao zilizoenea sehemu mbali mbali za Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.